NAIBU Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman alisema matarajio ya kuwapatia wananchi huduma zilizo bora za afya popote walipo ndio dhamira kuu ya Wizara zote za afya za Tanzania Bara na Zanzibar.
Hayo aliyasema leo huko katika ukumbi wa Ngalawa Beach Resort wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mrejesho wa maamuzi na maazimio ya mkutano mkuu wa 71 wa Afya Ulimwenguni .
Alisema Huduma za afya zinahitajika kuwafikia wananchi hivyo ili kufikia jitihada hizi Serikali zetu mbili hizi zimepiga hatua kubwa kuhakikisha kila sehemu zinawafikia walengwa bila matatizo yeyote na kwa urahisi.
Aidha alisema baada ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964 nchi yetu imekuwa ikichukuwa kila jitihada ili kufikia malengo yaliyotarajiwa , hivyo nchi yetu imekuwa ni moja kati ya nchi chache Barani Afrika , zenye mtandao mzuri wa miundo mbinu ya Afya.
Amewahakikishia wananchi kuwa sasa huduma za Afya za msingi zinapatikana katika masafa yasiozidi kilomita nne hadi tano hili ni jambo jema na tunapaswa kujipongeza.
Pia alisema Wizara na Serikali imeweka kipaumbele kwa ujumla kuziimarisha zaidi huduma hizi hasa katika maeneo na makundi maalum yakiwemo ya akinamama , watoto , walemavu na wengine wenye mahitaji maalum.
“Serikali imedhamiria kuziimarisha huduma za Afya nchini kwa watu wa aina zote ili waweze kufaidika na fursa hizo”. Alisema Naibu Waziri huyo.
Alisema mipango tuliyonayo katika kuimarisha Afya za jamii ni lazima kuangalia zaidi namna ya kuimarisha kinga ya maradhi yanayotuathiri kila siku , yakiwemo ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza .
Alielezea kinga ni bora kuliko kutibu hivyo ni vyema kuwekeza nguvu zaidi kwenye kinga kuliko kusubiri gharama kwa matibabu hapo baadae.
Vile vile alisema maradhi kama polio , surua, kipindupindu, malaria na mengine yanahitaji na mipango sahihi ya kupambana na kuimarisha viwango vya mafanikio na hatimae kuyaondosha kabisa katika jamii , hili linawezekana tujitahidi kutimiza wajibu wetu.
Aidha alisema shirika la Afya Duniani WHO linahakikisha watu zaidi ya billion moja wananufaika huduma za afya , billion moja wanalindwa na dharura za afya na billion moja wanafurahia afya bora na ustawi mzuri wa maisha yao.
Nae Naibu Waziri wa Wizara ya Afya Tanzania Bara Dkt Faustine Ndegulile alisema anaridhishwa na mashirikiano yaliyokuwepo kati ya wizara za Afya hizi mbili kwa kwenda sambamba kuwajali wananchi wake katika upatikanaji mzuri wa huduma za Afya.
Alisema katika masuala ya Afya tunasaidiana , tunafundishana kwa lengo la kukuza sekta hii ya Afya kwa madaktari wa Zanzibar na Tanzania Bara ili kuweka kufikia katika malengo na mkakati uliyokusudiwa .
Pia alipongeza Zanzibar jinsi ilivyopiga hatua nzuri katika kudhibiti malaria, na kusema mipango zaidi ya msingi yanaanza kufanyika ili kufikia kiwango kilokusudiwa, pia kuhakikisha dawa zinapatikana zinapatikana katika sekata zote mbili.
Sambamba na hayo Afisa anayesimamia Malaria , Ukimwi , na Kifua Kikuu katika Shirika la Afya Duniani WHO Dr Ritha Njau alisema analipongeza shirika hilo kwa kuweza kudhibiti malaria kwa kutoa elimu ya wananchi kulalia vyandarua tayari vimetiwa dawa.
Vile vile aliwataka wananchi wakipata homa waende kupima kwa vile homa zote sio malaria na hasa hivi sasa kasi za homa za malaria zimepungua .
Alielezea lengo la mkutano huu ni kuwapa marejesho wananchi ambapo mara moja kwa mwaka hukutana na kupanga mikakati kwa Bara na Visiwani.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Harus Said Suleiman akifungua Mkutano wa Marejesho wa Maamuzi na maazimio ya Mkutano Mkuu wa (71) wa Afya Ulimwenguni katika Ukumbi wa Hoteli ya Ngalawa Mjini Zanzibar.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Ulimwenguni Tanzania (WHO) Dkt. Adiele Onyeze akizungumza katika Mkutano wa Marejesho wa Maamuzi na Maazimio ya Mkutano Mkuu wa (71) wa Afya Ulimwenguni katika Ukumbi wa Hoteli ya Ngalawa Mjini Zanzibar.
Naibu Waziri wa Afya Tanzania faustine Ndugulile, akionesha kipeperushi cha Mpango kazi kilichoandaliwa na Wizara ya Afya Tanzania katika Mkutano wa Marejesho wa Maamuzi na Maazimio ya Mkutano Mkuu wa (71) wa Afya Ulimwenguni katika Ukumbi wa Hoteli ya Ngalawa Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Marejesho wa Maamuzi na Maazimio ya Mkutano Mkuu wa (71) wa Afya Ulimwenguni katika Ukumbi wa Hoteli ya Ngalawa Mjini Zanzibar.
Picha ya pamoja
Picha na Abdalla Omar Maelezo - Zanzibar.
Post a Comment