Wakati taasisi ya TWAWEZA ikipewa siku saba kujieleza ni kwanini isichukuliwe hatua za kisheria kwa kutoa matokeo ya utafiti bila ruhusa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), imesema kuwa imesikitishwa na kusambaa kwa barua hiyo mtandaoni.
Mara baada ya kusambaa kwa barua ya TWAWEZA iliyoandikwa kutokea COSTECH, Kaimu Mkurugenzi wa tume hiyo Dkt. Amos Nungu amesema kuwa baada ya kufuatilia barua hiyo waligundua kuwa ni yao.
“Baadaya kufanya uchunguzi tuligundua kuwa barua inayosambaa mitandaoni ni yetu tulioiandika kwenda TWAWEZA, tunasikitika kuona mawasiliano halali ya kiofisi yanapelekwa mitandaoni hata kabla ya kujibiwa”, amesema Dkt. Nungu.
Dkt. Nungu amesema kuwa COSTECH pekee ndio chombo cha kutoa ushauri katika masuala yote yanayohusu sayansi, teknolojia na uvumbuzi na moja ya majukumu yake ni kusajili na kutoa vibali vya tafiti zote za muda mfupi na mrefu zinazofanywa nchini.
Mwishoni mwa wiki iliyopita TWAWEZA ilitoa ripoti ya utafiti wa sauti za wananchi ukieleza hali ya siasa nchini, ambapo utafiti ulionesha kuporomoka kwa ukaribu wa wananchi na viongozi wa vyama vya siasa.
Post a Comment