WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezindua Muongozo wa Ujenzi wa viwanda ambao utatumiwa kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kwa lengo la kufanikisha Tanzania ya viwanda.
Uzinduzi wa muongozo huo wa ujenzi wa viwanda nchini ameufanya jana wakati anafungua rasmi Maonesho ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia muongozo huo alisema unatoa maelekezo katika kuhakikisha ujenzi wa viwanda unatekelezwa na kushauri wote wanaohusika na muongozo huo kuutumia vema.
“Muongozo wa ujenzi wa viwanda upo kwenye kijitabu hiki kidogo lakini kimefafanua kwa kina nini maana ya kiwanda na ili kiwepo kiwanda kitu gani ambacho kinatakiwa kufanyika.
“Kuna dhana ambayo imejengeka kwa baadhi ya wananchi , unapozungumzia kiwanda wanadhani labda uwe na jengo kuubwa na mashine ndani.Kumbe haiko hivyo na kupitia muongozo huu ambao nimeuzindua leo unafafanua vizuri,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa .
Alisisitiza lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha inatekeleza ujenzi wa viwanda ambao utatoa fursa ya kuendelea kwa uchumi na kutoa ajira kwa watanzania walio wengi.
Pia alihimia ujenzi wa viwanda ambao utakwenda sambamba na viwanda ambavyo vitatumika kuzalisha malighafi kwa ajili ya kutumia kwenye viwanda na kwamba ili kufanikisha hilo iko haja ya kuwekeza katika sekta ya kilimo.
“Serikali ina nia ya dhati ya kuendeleza kilimo nchini na Juni 4 mwaka huu umefanyika uzinduzi wa mpango wa pili wa kuendeleza kilimo nchini,”alisema.
Post a Comment