
Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Jakaya Kikwete
****************
Na Mwandishi Wetu,
Dodoma
MWENYEKITI wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka
viongozi wa chama hicho kukipigania chama ipasavyo kwa masuala ya kisiasa na
kuacha kutegemea Jeshi la Polisi na Serikali kuingilia masuala ya kisiasa. Rais
Kikwete ameyasema hayo usiku huu alipokuwa akifunga mkutano Mkuu wa CCM Taifa
mjini hapa uliomalizika majira ya saa tano usiku.
Alisema viongozi wa
chama wanatakiwa kukisemea chama bila kuchoka hasa kwa masuala ya kisiasa na
kuacha kutegemea viongozi wa Serikali na wakati mwingine vyombo vya dola
kuingilia masuala ya kisiasa. Alisema yapo maneno mbalimbali ya kipuuzi ambayo
yamekuwa yakitolewa na wapinzani dhidi ya CCM, ambayo yanapaswa kujibiwa na
viongozi wa CCM wenyewe na si vinginevyo.
Alisema tabia ya baadhi
ya viongozi hao kusikia hoja za wapinzani zikitupiwa ndani ya CCM huku wao
wamekaa kimya na pengine kuhoji kwanini viongozi wa Serikali hawachukui hatua
hazina msingi, hivyo wanapaswa kujibu hoja hizo kisiasa na si kutegemea vyombo
vingine.
“Tusitegemee Polisi na
Serikali kutusaidia kazi za siasa…mambo ya siasa yanajibiwa na wanasiasa
kisiasa, naomba twende tukakisemee chama hili hatulifanyi mara nyingi…tufanye
kazi ndani ya chama na nje ya chama,” alisema Kikwete katika hotuba yake ya
kufunga mkutano huo.
Aidha aliwataka viongozi
wa chama kukijenga chama kuanzi ngazi ya chini (kwenye mashina na matawi), ikiwa
ni pamoja na kujenga utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi na wanachama ili
wasaidie kuzifikisha ngazi husika kuwapuzia mzigo wananchi. Aliwataka viongozi
na wana CCM kuendelea kutekeleza mradi wa kukiimarisha chama, ikiwa ni pamoja na
kuendelea kuleta mageuzi ndani ya chama ili kukiimarisha chama.
“Tunaondoka leo hapa
twendeni tukazibe nyufa za uchaguzi, kuondoa mgawanyiko na mambo mengine ya
kipuuzi…,” alisema Mwenyekiti huyo wa CCM aliyechaguliwa tena kwa kishindo na
wajumbe. Aliwahakikishia kuwa chini ya uongozi wake atahakikisha CCM inashinda
tena kwa kishindo Tanzania Bara na Visiwani uchaguzi mkuu 2015.
Akizungumzia utendaji wa
Serikali ya CCM alisema itaendelea kufanya kazi zake kwa uwazi ili kujenga
uaminifu kwa wananchi; na kuongeza kuwa hivi karibuni atahakikisha kila waziri
anajitokeza kwenye vyombo vya habari na kuzungumza kinachoendelea wizarani kwake
pamoja na kujibu maswali ya wananchi baada ya kujieleza.


Post a Comment