Lionel Messi |
Cristiano Ronaldo |
Andres Iniesta |
Nyota wa Barcelona, Lionel Messi
na Andres Iniesta na wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo walitangazwa kuwamo
katika orodha ya wachezaji watatu watakaochuana kuwania Tuzo ya Mwanasoka Bora
wa FIFA (FIFA Ballon d'Or) katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo
nchini Brazil.
Muargentina Messi ameshinda tuzo
hiyo, zamani ikijulikana kama Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia, katika
kipindi cha miaka mitatu iliyopita na sasa anapewa nafasi kubwa ya kushinda tena
baada ya kuendelea na kasi yake ya kufunga magoli
‘atakavyo’.
Messi na Ronaldo ambaye pia
hufunga magoli kama mvua, mara kwa mara wamekuwa wakibishaniwa kuwa ni nani
mkali zaidi ya mwingine kati yao na mwaka huu hauna tofauti kwani wanaonekana
kuchuana vikali zaidi katika kila wiki.
Kocha wa Ronaldo katika klabu ya
Real Madrid, Jose Mourinho, alisema hivi karibuni kwamba itakuwa ni kosa la
jinai ikiwa mchezaji wake hatashinda Tuzo ya Ballon d'Or kwa mara ya pili, ikiwa
ni baada ya maoni kutoka kwa kocha wa Barcelona, Tito Vilanova aliyemuelezea
Messi kama "mchezaji mkali kuliko wote duniani, kwa tofauti kubwa kulinganisha
na wengine ".
"Kama Messi ndiye bora zaidi
duniani, Ronaldo ni bora zaidi ulimwenguni. Itakuwa ni kosa la jinai ikiwa
Ronaldo hatashinda Tuzo ya Ballon d'Or," Mourinho alisema Oktoba, muda mfupi
baada ya mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ureno kuwa mchezaji wa kwanza kuwahi
kufunga magoli katika mechi sita mfululizo za 'Clasico', ambazo huwakutanisha
mahasimu wa jadi Barcelona na Real Madrid.
Messi alifunga magoli 50 katika
La Liga, Ligi Kuu ya Hispania msimu uliopita, manne zaidi ya Ronaldo, na
ameshafunga magoli 82 katika mwaka wa kalenda hadi sasa, yakibaki magoli matatu
kabla ya kuifikia rekodi ya magoli 85 iliyowekwa na Gerd Mueller mwaka
1972.
Hata hivyo, Ronaldo ambaye ni
mshindi wa tuzo hiyo mwaka 2008 alikuwa mhimili wa Real Madrid katika safari
yake ya kutwaa taji la Ligi Kuu ya Hispania msimu uliopita na pia kuisaidia
Ureno kufika nusu fainali ya michuano ya Euro.
Iniesta ndiye mchezaji pekee kati
yao aliyetwaa taji la Kombe la Dunia na mataji mawili ya Euro akiwa na timu yake
ya taifa ya Hispania.
Kama Messi atashinda tuzo hiyo
mjini Zurich Januari 7, atakuwa mwanasoka wa kwanza kushinda tuzo hiyo mara nne
mfululizo.
Wanaowania Tuzo ya Kocha Bora wa
Mwaka wa Dunia ni kocha wa timu ya taifa ya Hispania, Vicente del Bosque, kocha
wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola na Mourinho.
Alex Morgan na Abby Wambach wa
timu ya taifa ya Marekani na Mbrazil Martha wametajwa katika orodha ya nyota
watatu watakaowania Tuzo ya FIFA ya Mwanasoka Bora Mwanamke wa Mwaka wa
Dunia.
Uteuzi huo umetokana na kura
ambazo zimepigwa na manahodha na makocha wa timu za taifa za soka za wanaume na
wanawake, pamoja na vyombo vya habari teule.
Post a Comment