Featured
    KWA HABARI NA MATANGAZO EMAIL : pbuyegu2@gmail.com ... Get a superior results by advertising with us by E- Mail us pbuyegu2@gmail.com We will bring Your Business to Light

    Featured Posts

Loading...

Lowassa taja mali umalize utata huu

VYOMBO mbalimbali vya habari vilimkariri Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, akisema kuwa hana utajiri wa fedha kama watu wanavyomzushia isipokuwa ana utajiri wa watu.
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli, alitoa kauli hiyo katika Kanisa la Moravian Tanzania Usharika wa Ruanda, wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa hosteli ya wanachuo wa kike wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji mkoani Mbeya.
Alisema kuwa amekuwa akisingiziwa mara nyingi kuwa yeye ni tajiri jambo ambalo si kweli bali utajiri alionao ni wa watu ambapo anaamini kuwa hawezi kufilisika na kwamba ataendelea kuchangia kwenye harambee.
Tunakubaliana kwa kiasi fulani na kauli ya Lowassa kuwa huenda akawa anazushiwa kama anavyodai mwenyewe, lakini ili kumaliza mzizi huo wa fitina, ni kujitokeza hadharani na kutangaza mali zake anazomiliki.
Tunashauri hivyo huku tukikumbuka ujasiri aliouonyesha Mbunge mwenzake wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), wa kutangaza mali zake waziwazi ili kuondoa utata kwa wale waliokuwa wakimtuhumu kwa ukwasi mkubwa.
Lowassa bila shaka anakumbuka vyema wakati wa utawala wa awamu ya tatu, chini ya Rais Benjamin Mkapa, ulitangazwa utaratibu wa viongozi kutaja mali zao ambapo Rais alikuwa wa kwanza kufanya hivyo akifuatiwa na mawaziri wasiozidi watatu.
Lakini kuonyesha kuwa viongozi wetu bado hawako wazi hata pale wanapotuhumiwa uongo, wanashindwa kujitokeza kujitetea kwa kutoa vielelezo, ndivyo alivyofanya hata Rais mstaafu Mkapa kwani wakati wa kustaafu hakuweza kutangaza tena mali zake licha ya tuhuma kibao za kujilimbikizia mali zinazomkabili hadi leo.
Ni katika mlolongo kama huo, hatuoni kama malalamiko ya Lowassa yanaweza kumsaidia chochote ikiwa hatajitoa kwa ujasiri kuanika mali zake kama alivyofanya Zitto.
Wahenga wanasema penye ukweli, uongo hujitenga, hivyo hata Lowassa kama amebaini kuwa tuhuma za ukwasi zinazoelekezwa kwake ni za uongo, ni bora akasafisha jina lake kwa kujitokeza mbele ya umma na kuweka bayana ukweli.
Lowassa ni mmoja wa vigogo wa CCM wanaotajwa kuwa wagombea urais mwaka 2015, hivyo ikiwa ataacha kulalamika na akajitokeza hadharani kutaja mali zake ili kuondoa utata, hakika atajijengea heshima kubwa mbele ya jamii.

chanzo: Tanzania Daima
Download Our App

Post a Comment

CodeNirvana

BLOG RAFIKI

© Copyright EMMANUEL SHILATU - BREAKING NEWS BLOG
Back To Top