|
|
SIKU moja baada ya Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, kuibana serikali
akiitaka ifafanue juu ya upotevu wa sh bilioni 86 za kununulia mafuta ya
kuendeshea mitambo ya umeme, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo, amekwepa kuzungumzia suala hilo.
Wakati Waziri Muhongo akikwepa, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi, na
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Jenerali mstaafu Robert Mboma, nao
walishindwa kutoa ufafanuzi.
Katika taarifa yake juzi, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Kaskazini
(CHADEMA), akinukuu taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) iliyobaini upotevu wa mabilioni hayo pamoja na mambo mengine alimtaka
Waziri Muhogo aeleze hatua alizochukua baada ya kukabidhiwa taarifa hiyo kuhusu
maofisa waandamizi wa wizara waliohusika na wizi huo.
Hata hivyo katika hatua ya kushangaza, Waziri Muhongo, alipotafutwa kwa njia
ya simu ili azungumzie juu ya upotevu huo wa mabilioni ya shilingi, alisema hana
cha kujibu na kwamba taarifa hizo yeye hajazisoma.
Alipotakiwa kuelezea hatua alizozichukua yeye kama waziri dhidi ya wizi huo,
Prof. Muhongo, hakuwa tayari bali alisema yeye sio mtu wa kulumbana na kwamba
kama kuna fedha zimeibiwa kuna taratibu za serikali.
“Tuongee mambo ya maendeleo, kuna wengine kulumbana ni kazi yao; sisi wengine
taaluma zetu sio hizo,” alisema Prof. Muhongo.
Mapema gazeti hili lilimtafuta Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi,
kuzungumzia taarifa hizo bila mafanikio.
Zitto katika taarifa yake mbali na Wizara ya Nishati na Madini pia alimtaka
Waziri wa Fedha na Uchumi aueleze umma juu ya kiwango cha fedha ambacho Hazina
imetoa kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya umeme wa dharura kati ya Novemba
2011 na Oktoba 2012.
Alipotafutwa, Waziri wa Fedha, William Mgimwa, kuzungumzia juu ya suala hilo,
simu yake iliita bila kupokelewa na hata alivyotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi
pia hakujibu.
Juzi, Zitto alibainisha juu ya kuwapo kwa ripoti zinazoonyesha kuwa kuna
kikundi ambacho kazi yake kubwa ni kujifaidisha binafsi na mpango wa umeme wa
dharura kupitia kwenye ununuzi wa mafuta mazito ya mitambo ya IPTL.
Alisema juhudi zilizofanywa na Kamati ya Bunge ya Hezabu za Mashirika ya Umma
ambayo yeye ndiye Mwenyekiti wake, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John
Mnyika, na aliyekuwa Mwenyekiti wa Nishati na Madini, January Makamba, za kutaka
uchunguzi juu ya suala hilo ufanywe, hazikuzaa matunda.
Katika kutafuta kiini cha upotevu, kwa mara nyingine, wa mabilioni ya
shilingi TANESCO, gazeti hili lilimtafuta Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Jenerali
mstaafu Robert Mboma, bila mafanikio.
Hata hivyo, alipopigiwa Makamu Mwenyekiti wake, Victor Mambalaswa, alisema
yuko jimboni na kwamba taarifa hiyo ya CAG kuhusu upotevu wa mabilioni hayo
haijafika TANESCO.
“Kama kuna mtu kaiona hiyo taarifa itakuwa serikalini lakini TANESCO bado
haijafika,” alisema Mwambalaswa.
Kwa upande wake Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, Mnyika, alisema anaungana
na Zitto kuwataka viongozi hao wa serikali watoe kauli kwa umma akiwamo CAG na
Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA).
Alisema iwapo kauli hazitatolewa kwa wakati atatoa nyaraka na majina ya
wahusika.
Mnyika alisema alichoeleza CAG kwenye taarifa yake kama ilivyonukuliwa kwenye
gazeti la The East African la Novemba 24-30 kuhusu dola milioni 54 (bil. 86) ni
sehemu tu ya tuhuma za ufisadi zinazotokana na ukiukwaji wa sheria ikiwemo ya
ununuzi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme.
“Lakini ukweli kuwa tuhuma za ufisadi, Waziri Muhongo, Waziri Mgimwa na
Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO Jenerali Mbona wanapaswa kutoa kauli kurejea
taarifa ya Zitto ya jana na taarifa yangu ya Novemba 23 mwaka huu,” alisema
Mnyika.
chanzo: Tanzania Daima
|
|
on Monday, November 26, 2012
Post a Comment