Waziri wa Ujenzi, Dk John
Magufuli
UTEKELEZAJI wa zoezi la
kukamata watumishi wa Serikali wanaotumia namba za kiraia kwenye magari ya umma
kinyume cha sheria na utaratibu, unasuasua kutokana na kuwapo kwa taarifa za
kutatanisha kuhusu kufanyika kwa kazi hiyo.
Taarifa zilizopatikana
zinaeleza kuwa tangu Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli atangaze kufanyika kwa
zoezi hilo akishirikiana na polisi, baadhi ya maofisa wa Serikali walibadilisha
namba kimyakimya bila kutolewa taarifa yoyote.
Chanzo chetu cha habari
kutoka Wizara ya Ujenzi, kimeeleza kuwa katika kazi hiyo, Dk Magufuli alitaka
liwe linatangazwa na kufanyika mara moja.
Kilisema, badala yake
inafanyika kwa siri na hakuna taarifa zinazotolewa waziwazi juu ya
utekelezaji.
“Sijui nini
kimetokea, tunaona zoezi liko kimya taarifa hazieleweki, tulisikia kuwa taarifa
kuhusu zoezi hilo lilikuwa limeandaliwa na wizara, lakini mpaka sasa haijatolewa
na hakuna kitu kinaendelea, nadhani kutakuwa kuna kitu kimetokea,”kilisema
chanzo hicho
na
kuongeza:
“Kila mtu wizarani
ukimuuliza kuhusu zoezi hilo haelewi kinachoendelea.”
Lakini taarifa
zilizopatikana kutoka vyanzo vingine vya habari zilieleza kuwa karibu magari 400
yamejiandikisha kupata namba za Serikali tangu zoezi la kakamatwa
litangazwe.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Jerryson Lwenge alipoulizwa juu ya zoezi hilo alisema kuwa atafutwe
naibu katibu mkuu wa wizara hiyo, John Ndunguru kwa kuwa ndiye anashikilia ofisi
ya katibu mkuu kwa sasa.
“Sisi tupo
Kenya kwenye mambo ya Afrika Mashariki mtafute naibu katibu mkuu ndiye anayeweza
kukupa taarifa,” alisema Lwenge.
Hivi karibuni, Naibu
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, John Ndunguru alivieleza vyombo vya habari kwamba
Serikali iliweka utaratibu unaozuia matumizi ya namba za kiraia kwenye magari
yake isipokuwa kwa kibali maalumu.
Alisema kuwa hali ya
kuzuia namba hizo iliibuka baada ya kubainika kwamba kupitia namba hizo, magari
ya umma yanatumika vibaya na baadhi
kupotea.
Kamanda wa Kikosi cha
Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga alisema Waziri alitarajiwa kutoa
ripoti jinsi zoezi hilo linavyoendelea kwa kuwa Waziri mwenyewe ndiye anatakiwa
kuzungumzia suala hilo.
Alisema zoezi la
ukamataji magari linaendelea kwa muda wa miezi mitatu mfululizo lakini hakusema
idadi ya magari yaliyokamatwa hadi hivi
sasa.
Post a Comment