Na: Albert Sanga, Iringa.
Miezi ya karibuni kule nchini Marekani askari walipambana na waandamanaji waliokuwa wakilalamika kuongezeka kwa pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho. Mara kadhaa waandamanaji hao wamejaribu kuandamana kupitia njia mbalimbali, ikiwemo ile ya kukutanika kwenye daraja la mto Missisipi; lakini mara zote wameambulia kufurumushwa na polisi.
Waandamanaji hao ambao wamekuwa wakijitambulisha kama masikini wanalalamika kuwa rasilimali za taifa la Marekani zinawanufaisha watu wachache. Wanalalamika kuwa serikali haiwajali watu masikini, wanalilia upatikanaji wa ajira pamoja na maisha mazuri.
Rais wa Marekani Barrack Obama ambaye ametetea kiti chake katika uchaguzi wa mwaka huu; safari hii aliamua kuelekeza kampeni na sera zake kwa ajili ya kuwaokoa masikini na watu wa kipato cha chini huko marekani. Sote tumeshuhudia namna alivyombwaga mshindani wake Mitt Romney kupitia sera zake za kupunguza kodi na kuwakumbuka masikini
Maandamano haya ya masikini wa Marekani pamoja na mgogoro wa madeni kwa mataifa yanayofadhili bajeti za nchi masikini ni masomo muhimu sana kwa taifa letu. Sasa tunabaini kuwa matatizo yanayotuhenyesha hapa nchini yameshakuwepo huko kwa 'walioendelea'.
Ukosefu wa ajira na kupanda kwa gharama za maisha kumezitingisha na kuzivuruga nchi za Magharibi. Ni huko tulikojua kuwa kuna neema, huku tukiwabeza watawala wetu kuwa wamekuwa wavivu wa kujifunza kutoka kwa hao, wakubwa.
Kimsingi kati ya mataifa masikini (ikiwemo Tanzania) na mataifa tajiri, linapokuja suala la ukosefu wa ajira na maisha magumu tunatofautiana katika fikra na tafsiri ya matatizo hayo. Katika nchi zilizoendelea wanapotaja ajira wanajumuisha kuajiriwa na kujiajiri. Kwa wenzetu dhana ya kujiajiri ilitangulia miaka mingi sana kutokana na ubepari na imetawala kuzidi hata kuajiriwa.
Wakati wao wanalia kuwa hakuna ajira (kujiajiri ama kuajiriwa) kutokana na uchafuzi wa mazingira, ukosefu wa ardhi na uhaba wa masoko sisi tunalia kinyume chache. Kwa ufupi wanalia ufinyu wa fursa kwa sababu watu walishajanjaruka siku nyingi! Hapa nchini kilio cha ajira kipo tofauti.
Maelfu ya wasomi na wasiosoma unapowasikia wanalia ukosefu wa ajira basi wanakuwa wakimaanisha kuajiriwa. Bado tuna asilimia ndogo sana ya vijana wasomi ambao wanaamini na kuamua kujiajiri moja kwa moja bila hata kupitia kuajiriwa. Wakati wenzetu huko 'majuu' wanatamani kujiajiri lakini wanakosa fursa na rasilimali, sisi huku 'hatujisomi' wakati tumezungukwa na neema lukuki.
Sababu zinazotolewa na wasomi wengi kuhusu kushindwa kwao kujiajiri ndizo zinanisukuma kuona kuwa ipo haja ya kuwafundisha wasomi wetu jinsi ya kujiajiri. Ingawa kuna sababu nyingi lakini iliyo maarufu ni ukosefu wa mitaji.
Ninachofahamu mimi ni kuwa kabla ya mitaji kuna mambo yanatakiwa kutangulia. Jambo la kwanza ni mfumo wa kifikra kuhusu suala lenyewe la ukombozi wa kiuchumi (mindset toward financial freedom). Mtu akishaamini kuwa anaweza kujikomboa kiuchumi ndani yake kunatokea kujiamini na kuthubutu ambako huambatana na mtiririko wa mawazo (constant flow of ideas).
Kwa hiyo tatizo la msingi tulilo nalo katika nchi yetu kwa sasa utabaini kuwa sio maisha magumu na wala sio ukosefu wa ajira isipokuwa ni mfumo mbaya wa kifikra ambao ni tegemezi kwa serikali. Kila anaesoma anawaza kuajiriwa na kwa sababu ajira (za kuajiriwa) ni chache wanapata wachache na waliobakia wanabaki kuwa mzigo ama hatari kwa taifa.
Ni mzigo kwa taifa nchi inapokuwa imetumia mabilioni kuwasomesha wasomi vyuoni halafu wanaranda mitaani bila kuzalisha kwa sababu hawana ajira. Rais Jakaya Kikwete amepata kutahadharisha kuwa vijana wasio na ajira ni bomu linalosubiri kulipuka (kama halitateguliwa nadhani zima moto iandaliwe!)
Hatari inayolipata taifa hili (kutokana na sumu ya ukosefu wa ajira) ni kuzalisha wasomi bila uwiano wa mahitaji yaliyopo katika jamii. Kinachotokea kwa sasa, wasomi wanapotafuta kazi hawatafuti kutokana na taaluma zao, wanachojali ni mradi mkono uende kinywani. Aliesomea mambo ya ustawi wa jamii unamkuta anafundisha sekondari!
Aliesomea sheria unamkuta ni 'mhesabu fedha benki'. Aliesomea mambo ya biashara na uchumi unamkuta amejishikiza kwenye NGOs ya masuala ya Ukimwi. Uzalishaji mali katika taifa unadorora kwa sababu tumeweka watu sahihi (wasomi) katika maeneo yasiyo sahihi. (wanapofanya kazi ambazo sio za taaluma zao). Hili naomba niliache kwa sababu lina mwelekeo wa kisera zaidi; narudi katika ngazi ya mtu mmoja mmoja.
Ufumbuzi wa fikra za kiutumwa (wrong mindset) upo katika kuzibadilisha fikra za wahusika (hapa tunawaongelea maelfu ya wasomi wanaohitimu kila mwaka pasi kuwa na ajira). Fikra kikawaida inabadilishwa kutokana na kile kinachoingia katika ubongo wa mtu iwe kwa kusoma, kuona ama kusikia..
Watu wa mifano (role models) wa wasomi wetu wengi ni watu waliopo katika ajira za kuajiriwa; wanawatazama wanavyoendesha magari mazuri yenye nembo za STK, STJ, PT, DFP na nyingine kama hizo; wanayatamani mahekalu wanayoishi na hivyo katika fikra zao kunaaminika kuwa mafanikio ya kiuchumi ni "Kupata ajira yenye mshahara mkubwa na marupurupu mengi".
Ndio maana hakuna kitu kinachonisikitisha ninapoona watu wanakimbizana kwenda kuongeza elimu (shahada, sahada za uzamili na shahada za uzamivu) wakiwa na lengo la kuongezewa viwango vya mishahara yao. Wasichokielewa ni kuwa haiwezekani mtu kuwa tajiri kupitia mshahara peke yake-kwa mishahara ya hapa Bongo!. (nasisitiza, mshahara peke yake!).
Kiukweli hali imebadilika, sio rahisi kwa kila mhitimu wa chuo kikuu kubahatika kupata ajira zenye hadhi ya kutembelea STK, STJ na nyingine achilia mbali ajira hata za mishahara midogo. Sasa kibarua kinachokuwepo hapa ni namna ya kuwatoa wasomi wetu kutoka hapo walipo kifikra na kuwaleta katika ulimwengu wa "Inawezekana kujikomboa kiuchumi kupitia biashara, ujasiriamali na kujiajiri kupitia miradi mbalimbali”
Wanaofanikiwa iwe katika siasa, biashara, ajira ama kiimani hawakabidhi jukumu la ustawi wao mikononi mwa wengine iwe ni serikali, jamaa ama marafiki. Huu mtindo wa kuangalia kila jambo na kurusha mzigo kwa serikali haututoi na kamwe hautawaokoa vijana wengi wanaokosa ajira. Badala ya kuongeza bajeti ama kutenga mafungu ya kuwakopesha tunatakiwa tuchukue hatua zingine zitakazopelekea wasomi hawa wajiajiri (nitaeleza katika makala zijazo).
Tunahitaji kuwafundisha vijana wasomi wawe na macho ya ndani kuona mambo kitofauti. Katikati ya migogoro waone masuluhisho na sio kuandamana! Ndani ya kuyumba kwa uchumi wazione fursa na sio kuwaza mapinduzi ya kisiasa! Vumbi la ukosefu wa ajira linapotimka wao wawashe mianga ya kutengeneza ajira.
Hawa wote wanakuwa wamefanikiwa kupata ustawi chanya wa kifikra. Ustawi wa kifikra hauji hivi hivi, unatafutwa kama vinavyotafutwa vitu vingine vya thamani. Ustawi chanya wa kifikra (positive mindset) ni mchakato wa muda mrefu unaojengwa kupitia utamaduni wa kitaifa, malezi ya kifamilia, mwingiliano wa kimataifa na juhudi binafsi za mtu kuitimiza ndoto ya maisha yake. Katika hatua hii ya juhudi za mtu binafsi ndipo hapa ambapo utamaduni wa kujielimisha kwa njia mbalimbali hasa usomaji wa vitabu ni jambo lisilokwepeka!
Pamoja na kwamba ipo haja ya jamii kushirikiana na wasomi (ambalo ni bomu linalojiandaa kulipuka na kutudhuru wote) kuwasaidia ama niseme kuwaelekeza namna ya kujiajiri, bado wasomi wetu wana changamoto ya kuanza utamaduni wa kujisomea na kudadisi mambo mbalimbali zaidi ya kusoma kwa kujibia mitihani.
Tumefika mahali ambapo hakuna uchaguzi tena; eidha ujielimishe, uchukue juhudi na kurekebisha hali yako ya kiuchumi na kijamii ama ukomae kutobadilika na ubaki kuwa mtu wa malalamiko huku ukisaidiwa na wanaharakati 'uchwara' wanaojaza fikra hasi na ujikute una kiu ya kuandamana kuliko kiu ya kubeba jembe na kwenda kulima.
Nihitimishe kwa kusema kuwa wasomi wetu wengi wanashindwa kujiajiri sio kwa sababu ya kushindwa kutunza mahesabu (ingekuwa hivyo wanaomaliza uhasibu wangekuwa mamilionea). Wala haitokani na kukosa mitaji (ingekuwa hivyo wengi wangefanya mambo ya msingi sana kupitia mikopo wanayoipata wakiwa masomoni). Na tena haisababishwi na maksi chache za darasani (ingekuwa hivyo wenye alama za juu kabisa wangekuwa wanamiliki makampuni makubwa).
Tatizo la wasomi wetu kushindwa kujiajiri linatokana na kutofunguka kifikra pamoja na mazoea ya kitamaduni na kimalezi yaliyopo katika mfumo wa elimu na maisha. Kwa kuwa tupo kwenye zama za hatari ambazo wenye nguvu pekee ndio wataishi (survival of the fittest) ni wakati muafaka sasa kuwapa mbinu, hamasa na mifano michache na iliyo hai ya vijana ambao wamefanikiwa katikati ya mazingira haya haya ambayo wengine wanasema hayawezekani.
Pia ni wajibu wa kila msomi kujikusanyia nguvu (nguvu ya maarifa huru ya kifikra yatakayokupa uhuru wa kiuchumi) ili kuweza kuishi. Ikumbukwe kuwa siku zote mlalamishi sio muwajibikaji na muwajibikaji ndiye hutokea kuwa shujaa!
Wasomi wetu wanahitaji ushindi wa kiuchumi na kifikra!
stepwiseexpert@gmail.com.
Post a Comment