Vipande hivyo vina jumla ya kilo 36.837 na thamani ya Sh. milioni 36.6 na nyara mbalimbali za serikali.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema jana kuwa watu hao walikamatwa katika maeneo mbalimbali katika Manispaa ya Dodoma na wengine katika Wilaya ya Chemba.
Alisema juzi majira ya jioni katika maeneo ya “Area A” Polisi waliwakamata watu wawili wakiwa na pembe za ndovu vipande vinane.
Aliwataja watu hao kuwa ni Tamba Bakar, Tamba Avanda (42) ambaye ni fundi baiskeli na Rajab Seleman (28), mkulima na mkazi wa Bahi Road.
Alisema watuhumiwa hao walikuwa wamehifadhi meno hayo katika begi wakiyasafirisha kwa pikipiki yenye namba za usajili T 408 BUJ, mali ya Tamba Avanda.
Misime alisema walipopekuliwa nyumbani kwao, Tamba alikutwa akiwa na risasi 15 za bunduki aina ya riffle, tochi ya kuwindia na leseni ya bunduki ya Rifle namba 70-95025.
Kwa mujibu wa Misime, mtuhumiwa huyo alidai kuwa bunduki hiyo aliikodisha mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la Peter Lugesha, mkazi wa kijiji cha Mambaka Kwa mtoro wilayani Chemba.
Alisema pia Polisi wakiwa katika doria majira ya saa mbili usiku katika eneo la Area “C’’, mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Mohamed, mkazi wa Air Port ambaye awali alikuwa akitafutwa na Polisi, alikimbia na kutelekeza mfuko uliokutwa na vipande 16 vya pembe za ndovu.
Kamanda huyo alisema pia juzi majira ya saa 10:00 jioni katika kitongoji cha Mambaka katika Kijiji cha Kubi wilayani Chemba, alikamatwa Galahenga Mahiya (27) akiwa na gobore.
Alisema gobore hilo lenye namba TB.1256 lililosajiliwa mkoani Tabora na alikutwa akiwa na baruti gramu 250, gololi 104, ngozi moja ya mnyama aina ya tandala na ngozi moja ya mnyama ajulikanaye kwa jina la karungu yeye.
Kamanda huyo alisema watu hao watafikishwa mahakamani baada ya kukamilika kwa upelelezi.
CHANZO: NIPASHE
Post a Comment