Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akijiandaa kukabidhi msaada wa Vitanda 38 pamoja
na Magodoro na Mashuka yake kwa Hoapitali Kuu ya Mnazi
Mmoja.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif akiwajulia hali watoto waliolazwa kupatiwa huduma katika
wodi ya ajali Mnazi Mmoja kabla ya kukabidhi msaada kwa ajili ya wodi
hiyo.
Balozi Seif akimkabidhi
Muuguzi Mkunga wa Wodi ya Watoto waliopata ajali Bibi Leluu Omar Said msaada wa
vitanda 14, magodoro na mashuka kwa ajili ya wodi hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif akifuatana na Waziri wa Afya Mh. Juma Duni Haji, Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Saleh Mohd Jidawi na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji
Wananachi Kiuchumi na Ushirika Mh. Haroun Ali Suleiman wakiangalia msaada wa
vitanda, magodoro na mashuka yaliyotolewa na msamaria mwema katika Hospitali Kuu
ya Mnazi Mmoja.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif akimpa pole mmoja wa wagonjwa wa wodi ya Mifupa aliyelazwa
kabla ya kukabidhi msaada wa vifaa vilivyotolewa na wasamaria
wema.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi Muuguzi dhama wa wodi ya Mifupa Bibi Afsa
Abdulla msaada wa vitanda 24, magodoro na mashuka kwa ajili ya wodi
hiyo.
Wafadhili na washirika wa
Maendeleo wameendelea kukumbushwa kuchangia huduma za afya kwa nia ya
kuwaondoshea mzigo wananachi pamoja na Serikali katika upatikanaji wa huduma
hiyo muhimu.
Kumbusho hilo limetolewa na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, wakati akikabidhi
Msaada wa Vitanda 28 pamoja na Magodoro, Mito na mashuka kwa ajili ya Wagonjwa
wanaolazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Msaada huo wa Vitanda
unaokadiriwa kugharimu shilingi za Kitanzania Milioni 12,000,000/- unazihusu
wodi ya Watoto wanaopata ajali, Wodi ya Mifupa ya wagonjwa wa Kiume pamoja na
chumba wanacholazwa wagonjwa wanaotumikia chuo cha mafunzo katika Hospitali Kuu
ya Mnazi Mmoja.
Akikabidhi msaada huo
uliotolewa na Wasamaria wema, Balozi Seif amesema bado Hospitali pamoja na Vituo
vya afya hapa Nchini vinahitaji kupatiwa misaada ili viweze kutoa huduma katika
kiwango kinachokubalika.
Amesema Serikali kwa upande
wake itaendelea kujitahidi zaidi katika kutafuta wafadhili sambamba na kuongeza
nguvu za upatikanaji wa vifaa vya huduma, lengo likiwa ni kuimarisha huduma za
afya mijini na Vijijini.
Msaada huo unafuatia ziara
ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliyoifanya katika sekta ya afya mwaka
uliopita na kushuhudia changamoto kadhaa zinazovikabili vituo vingi vya afya,
pamoja na Hospitali ukiwemo uhaba na uchakavu wa vitanda na magodoro ya
wagonjwa.
Wakipokea msaada huo kwa
nyakati tofauti Muuguzi Mkunga katika wodi ya Watoto Bibi Leluu Omar Said na
Muuguzi dhamana katika Wodi ya Mifupa ya Wagonjwa wa Kiume Bibi Afsa Abdulla,
wamewashukuru wafadhili hao kupitia Balozi Seif kwa msaada wao utakaosaidia
kupunguza matatizo yanayozikabili hospitali hiyo.
Wauguzi hao wakuu wa wodi
hizo wameahidi kwa pamoja kuvitunza Vifaa hivyo ili vidumu kwa muda mrefu kwa
vile changamoto hiyo lilikuwa kilio chao cha muda mrefu.
Hata hivyo wauguzi hao
wameiomba serikali kufanya utaratibu wa hifadhi zaidi ya magodoro hayo ili
yadumu zaidi suala ambalo Balozi Seif ameuagiza Uongozi wa Wizara ya Afya
kulifanyia kazi mara moja.
Mapema Balozi Seif alipata
fursa ya kuwatembelea wagonjwa waliolazwa katika wodi zilizofanikiwa kupata
msaada wa Vitanda, magodoro pamoja na Mashuka.
Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi anatarajiwa kutoa msaada kama huo hivi karibuni
katika Hospitali za Micheweni na Vitongoji Kisiwani
Pemba.








Post a Comment