Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Seth Kamuhanda.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Seth Kamuhanda amewataka Watanzania kuchangamkia fursa za ajira zitakazotokana na kuwepo kwa makao makuu ya Kamisheni ya Kiswahili upande wa Afrika Mashariki ambayo yatakuwa Zanzibar.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu huyo wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi na wizara kwenye kikao cha pili kilichofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
“Nchi uwanachama zimeridhia Tanzania kuwa makao makuu ya kamisheni. Taratibu za awali za kutia saini mkataba kuwa makao makuu kuwa Zanzibar unaendelea,”. alisema Katibu Mkuu huyo.
Alisema kuwepo kwa makao makuu hayo kutaongeza uwepo wa ajira , hivyo Watanzania wanatakiwa kujiandaa na ushindani juu ya suala hilo.
Aidha Kamuhanda aliwataka watumishi wa wizara hiyo wa sekta hizo kufanya kazi kwa bidii na uwajibikaji ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Aliitaka sekta michezo kufanya jitihada za kuzalisha wanamichezo bora kwenye maeneo wanayosimamia ili kuweza kuleta sifa katika taifa letu.