Kocha Mkuu wa Taifa Stars,
Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 21 kitakachoingia kambini Jumapili
(Februari 3 mwaka huu) kwa ajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Cameroon
(Indomitable Lions).
Akizungumza na Waandishi wa
Habari, Dar es Salaam leo (Januari 31 mwaka huu), Kim amesema mechi dhidi ya
Cameroon itakuwa kipimo kizuri kwake kwa sababu ni sehemu ya maandalizi kabla ya
kucheza mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Morocco itakayofanyika Machi
mwaka huu.
“Itakuwa mechi ngumu na
kipimo sahihi kwetu. Tuko tayari, tutacheza kwa staili yetu kwa sababu ni sehemu
ya maandalizi kabla ya mechi dhidi ya Morocco. Ni mechi nzuri kwa sababu
wachezaji wameonyesha wako tayari.
“Tumetoka kucheza dhidi ya
Zambia na Ethiopia. Lengo ni Taifa Stars kucheza fainali za AFCON 2015, kwa hiyo
mechi dhidi ya Cameroon ni sehemu ya mipango yetu kuhakikisha tunafika huko,”
amesema Kim ambaye amerejea nchini juzi kutoka Afrika Kusini kuzifuatilia timu
za Morocco na Ivory Coast zilizo kundi moja na Tanzania katika mechi za mchujo
za Kombe la Dunia.
Taifa Stars inayodhaminiwa
na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Morocco, Machi 24 mwaka huu Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam. Stars inashika nafasi ya pili katika kundi lake nyuma ya
Ivory Coast inayoongoza. Timu nyingine katika kundi hilo ni
Gambia.
Wachezaji aliowaita kwenye
kikosi chake ni makipa Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam) na Aishi Manula
(Azam). Mabeki ni Erasto Nyoni (Azam), Nassoro Cholo (Simba), Aggrey Morris
(Azam), Nadir Haroub (Yanga), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba) na
Issa Rashid (Mtibwa Sugar).
Viungo ni Amri Kiemba
(Simba), Simon Msuva (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa
Sugar), Salum Abubakar (Azam), Khamis Mcha (Azam), Athuman Idd (Yanga) na Mwinyi
Kazimoto (Simba). Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Simba), na Mbwana Samata na
Thomas Ulimwengu wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC).
Post a Comment