MWAKA 2013 ndiyo umeanza tupeane heri ya mwaka mpya kwa tuliobahatika kuuona. Wakati huu tukiuanza mwaka ni busara kujikumbusha kwa hoja baadhi ya mambo yatakayoendelea kutuathiri mwaka huu, kwa namna chanya ama hasi.
Mwaka uliopita, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) Ludovick Utoh na kamati tatu za kudumu za Bunge; Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kwa pamoja walibaini kwa kuainisha bungeni ufisadi na ubahirifu wa kutisha ambao ukiendelea kufunikiwa kombe mwaka 2013 ili mwanaharamu apite, basi hali ya uchumi na ustawi wa nchi vitakuwa taabani na wananchi hawatabahatika hata kuota ndoto ya maisha bora kwa kila Mtanzania.
Huko serikalini yawezekana watendaji na wasimamizi wa rasilimali za nchi wameamua pasi woga kujigawia nchi kwa manufaa binafsi na familia zao. Ndiyo! Haiwezekani kila siku watu hao hao wanatoa macho na kulaani ufisadi, sijui ubadhirifu lakini kila ripoti za ukaguzi zinapowekwa wazi, uozo ule ule unajirudia, tena kwa kiwango cha juu.
Pasi kuwapumzisha jela watendaji waitiao hasara nchi, nani atahanikiza maendeleo kwa wananchi? Halafu nani anawapa kiburi hasa mawaziri wanaoshindwa kazi lakini kujiuzulu ni hadi atishwe bosi wao kupoteza kazi! Wengine wamefikia hatua ya kuchokwa lakini wanaendelea kuwepo wizarani hadi leo! Wapo wasioogopa hata kujinunulia mahekalu ya ‘bei za kawaida’ kwa kiwango cha ‘dola’ lakini kujiuzulu inakuwa ngumu hadi waachwe kwenye uteuzi mwingine!
Wengi walipatwa na farijiko kiasi kwa uamuzi muhimu na uthubutu wa baadhi ya wabunge katika kusukuma mambo na hata kufikia hatua ya kukusanya sahihi zitakiwazo ili kutoa hoja bungeni ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, ambaye alikuwa ‘mtoto wa mkulima’ Mizengo Pinda, aliyechukua mikoba baada ya Edward Lowassa kujiuzulu ili kulinda maslahi ya CCM na nchi!
Yaonekana zama hizi za ubinafsi kifisadi na ulaji siasani, kujiuzulu ni dhambi. Hivi tujiulize, endapo Lowassa angekataa kujiuzulu kama ilivyo kwa mawaziri “kusikilizia” hatima zao badala ya kuchukua maamuzi magumu ingekuwaje? Nani angemlazimisha nguli Lowassa kujiuzulu kwa hali hii? Je, nchi ingekuwa bora zaidi pamoja na Lowassa ama imekuwa afadhali bila Waziri Mkuu mstaafu?
Kwanini iwe vigumu kujiuzulu uongozi pale kiongozi wa kuteuliwa (hata kuchaguliwa) unapoboronga ama kushindwa kazi! Unashindwaje kuachia ngazi wizarani, tena wizara nyeti kama ya elimu, pale unapovurunda kwa kiwango cha juu kabisa Kwanini basi mtu usilinde heshima yako kwa kuamua ‘kiroho safi’ kukaa pembeni badala ya kusubiri kuachwa pindi mabadiliko yatakapofanywa katika Baraza la Mawaziri? Kwani siasa siku hizi imegeuka kuwa ajira ya kudumu kwa ‘wanaobahatika’ kupewa ‘ulaji’.
Watawala wa Tanzania wengi wanapenda sana kulaani, kushutumu, kutoa matamko na maonyo. Haijalishi cheo, kila mwenye kuhisi anayo mamlaka huhakikisha sauti yake inasikika kupitia maonyo, vitisho vya ‘kuchukua hatua kali’ na yafananayo.
Utasikia mara waziri fulani amewalaani watendaji wanaojilipa posho kubwa; mara wabunge wameshutumu tabia ya wanaokeketa, au mkuu wa wilaya amewaonya wapinzani ama wabunge kuwa atawaweka mahabusu; na wengine wenye fursa za kuongea wamekosa hoja kiasi cha kufikia kujadili mavazi tu ya kinadada ilhali nchi inatota kimaendeleo.
Uko wapi basi utendaji na unenaji kwa masuala ya msingi kwa maendeleo ya nchi? Kwani hiki kisingizio cha maadili hakihusu ufujaji kifisadi unaoendelea huko mnakoita makazini?
Nakumbuka watu wengi waelewa walisikitika sana pale Mbunge wa Monduli alipojiuzulu Uwaziri Mkuu. Wengi tulijiuliza alimaanisha nini Lowassa aliposema tatizo ni uwaziri mkuu aliokuwa nao, lakini sasa ni wazi kwa jinsi waheshimiwa waliopo ‘makazini’ wanavyojiamini katika kazi zao pasi woga wala angalau kushtuka tu kutokana na kelele nyingi za wananchi wasioshawishika na utendaji wao.
Najua sasa kwa nini baadhi ya wasiojituma walivyofurahi Lowassa kung’atuka kwa kuwa walijua na wanajua endapo angeendelea kuwa bosi wao, ofisi ‘zisingetosha’ kwa wazembe, wabadhirifu na wapenda posho na starehe. Mfano uko wazi kule Wizara ya Uchukuzi ya Dk. Harison Mwakyembe, na Wizara ya Ujenzi kwa Dk. John Magufuli ‘kusivyotosha’. Nchi ingepata viongozi wabunifu na wachapakazi pasi kuhusishwa na urais 2015 hakika maisha bora kwa Watanzania yangekuwa na uhalisia.
Ya wahenga, “mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni” yafaa nukuliwa. Licha ya ile hotuba iliyowasilishwa kwa umahiri bungeni, ikifuatiwa na uamuzi mgumu, Lowassa katika suala la utendaji ni kichwa, hana masihara ya baraza la kahawa wala ‘longolongo’ tupu.
Mawaziri hawa wanaosikilizia badala ya kufanya kazi na wale wanaojihesabu hawawezi kuguswa hakika wasingefanya hivyo endapo Lowassa angekuwa Waziri Mkuu. Pia masuala mazito kama suala la maandamano ya kudai gesi yaliyofanywa na wananchi wa Mtwara yasingetokea ama kupita hivi hivi pasi yeye kulizungumza. Hilo kubali, kataa!
Sihitaji kuzitazama rekodi zake zote za awali kwa ulinganifu na za wengine, yatosha tu kuirejea miaka yake aliyohudumu kama Waziri Mkuu, achilia mbali hili la Richmond ambalo lina mengi na wengi ndani yake. Yako wapi maendeleo yaliyotarajiwa kupitia shule za kata na mengineyo!
Lowassa kama angekuwa bado ni ‘mtu mkubwa serikalini’ nisingetaraji ukimya huku maswali mengi yakihitaji na kusubiri majibu, tena ya haraka na uhakika. Nisingesubiri hoja ya Zitto kutaka nipigiwe kura ya kutokuwa na imani ili niwaelekeze mawaziri kuandika barua za kujiuzulu, kwa kuwa nisingetaraji mawaziri kuendelea ‘kusikilizia’ hatima zao badala ya kufanya kazi za nchi walizopewa au kujiuzulu mapema wakishindwa.
Zikiachwa siasa za maji taka na unafiki wenye wivu hasi, visasi, na visingizio, wote tutaipenda Tanzania. Ila kwa hali ilivyo na kwa kutilia maanani ongezeko la deni la Taifa kutoka Sh Trilioni 10.5 mwaka 2009/ 10 hadi Sh Trilioni 14.4 mwaka 2010/ 11, yaani ongezeko la asilimia 38, ni bora mara nyingi utendaji wa faida kwa nchi kuliko siasa za dhiki kwa wananchi.
Ni bora kwa Lowassa aliyejiuzulu kuliko wengi wenye haiba ya ‘kusikilizia’ huku wakiendeleza uborongaji kwa kiwango. Tumeambiwa kuwa miongoni mwa maeneo makuu kulikoripotiwa na CAG kukithiri wizi na ubadhirifu kuwa ni kwenye magari ya serikali kulikogharimu Trilioni 5! Bila shaka utendaji bora wa Dk. Magufuli utatoa kiwango tofauti kwa mwaka huu 2013.
Ubora wa kujiuzulu, ulazima wa kufukuza ama kufukuzwa, nguvu za umma, na njia zote za kuyafikia maendeleo yakini lazima vitumike mpaka hapo tutakaporidhia uthabiti na utayari katika maneno na matendo ya wanaopewa dhamana ya umma. Mpaka hapo, muda ndiye muamuzi.
Mwandishi ni Franklin Victor ambaye ni Mwanasheria na Mwanahabari, 0783 896 839.

Post a Comment