Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Mgana Izumbe Msindai akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kituo cha zamani cha mabasi mjini Singida, Msindai alikuwa akijitambulisha kuvunja makundi na kupokea kero mbalimbali za wananchi.
Baadhi ya wanaccm na wananchi wa Singida mjini wakimsikiliza kwa makini mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Mgana Izumbe Msindai (hayupo kwenye picha) wakati akihutubia.(Picha na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu.
Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wananchi wa mkoa wa Singida kwa ujumla, wameaswa kutumia mwaka huu mpya, kujiwekea malengo ya kufanya kazi halali kwa bidii na maarifa ili waweze kujiletea maendeleo makubwa zaidi kuliko yaliyopatikana mwaka jana.
Changamoto hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa Singida Mgana Izumbe Msindai, wakati akiutubia wananchi wa Manispaa ya Singida kwenye kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kituo kikuu cha mabasi cha zamani mjiniSingida.
Amesema kujituma kufanya kazi kwa bidii, maarifa na kwa malengo, ndio njia pekee inayoweza kumsaidia mwananchi ye yote kujikomboa kiuchumi na kupelekea kuishi maisha bora.
Akifafanua zaidi, Msindai amesema linapokuja suala la maendeleo, ni lazima itikadi za kisiasa ziwekwe pembeni, ili maendeleo endelevu ya mtu mmoja mmoja, wilaya, mkoa na hata taifa, yaweze kupatikana.
Msindai ambaye ni maarufu kwa jina la CRDB benki inayomjali mteja, ametumia fursa hiyo kuwashukuru wana CCM kwa kumchagua kwa kishindo kushika nafasi ya mwenyekiti CCM Mkoa.
Wakati huo huo, Msindai amesema kuwa wamekubaliana na manispaa ya Singida, kituo kikuu cha zamani cha mabasi, kuanzia sasa kitumike kwa mabasi madogo kushusha abiria hadi hapo manispaa itakapoanza kujenga kitega uchumi.