Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas akiongea na waandishi
wa habari mara baada ya kukamata madawa ya kulevya aina ya Mirungi viroba 202
katika eneo la Engikareti lililopo wilayani Longido Mkoa wa
Arusha.
Baadhi wa askari wa jeshi la
polisi wakiharibu madawa ya kulevya aina ya mirungi kwa kuikata kata na kisha
kuimwagia mafuta. Mirungi hiyo ilikamatwa katika eneo la Engikareti lililopo
katika wilaya ya Longido Mkoani Arusha.(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la
Polisi Arusha)
Jeshi la Polisi mkoani hapa
limewakamata watu wanne wakiwa na madawa ya kulevya aina ya mirungi. Watu hao
walikuwa na jumla ya viroba 202 vya madawa hayo ambayo yalikuwa kwenye gari aina
ya Mitsubishi Canter lenye namba za usajili T 306
BUN.
Akizungumza na waaandishi
wa habari nje ya jengo la Makao Makuu ya Jeshi hilo Mkoani hapa, Kamanda wa
Polisi Mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas aliwataja
watuhumiwa hao kuwa ni Joel Alfayo Lukumay (37), Rahim Azizi Gilla (35),
Ibrahimu Solomon Katambwei (40) na Musa Lazaro Mollel (38) wote ni wakazi wa
Mkoa wa Arusha.
Alisema
tukio hilo lilitokea leo saa 1:00 asubuhi katika eneo la Engikareti lililopo
wilayani Longido mkoani hapa. Aliongeza kwa kusema kwamba, mafanikio hayo
yametokana na taarifa toka kwa raia wema ambao waliwasiliana na jeshi hilo,
ambapo mara baada ya kupata taarifa hiyo waliweka mtego katika eneo hilo na
kufanikiwa kulikamata gari hilo ambalo lilikuwa linatokea nchi jirani ya
Kenya.
Kamanda
Sabas aliwashukuru wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa ushirikiano wao mkubwa
unaofanywa kwa jeshi hilo na kuwaomba waendelee kutoa taarifa za uhalifu na
wahalifu kwani kama wananchi wakiamua uhalifu unaweza ukapungua kwa kiasi
kikubwa.
Baadhi ya
waaandishi na askari waliokuwa kwenye eneo hilo walishuhudia viroba hivyo vikiwa
na majina ya watu pamoja na uzito wa kila mzigo huku wengine wakidai kwamba
inawezekana gari hilo huwa linabeba mizigo ya watu mbalimbali ambao wanakuja
kugawana mara baada ya kuingia Arusha Mjini.
Kutokana
na tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoani hapa linaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na
pindi upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma
zinazowakabili. Aidha taarifa za ndani ya jeshi hilo zinasema kwamba gari hilo
lilishawahi kukamatwa tarehe 16 mwezi Machi mwaka jana ambalo lilikutwa na
madawa ya aina hiyo na kesi yake ilikwishafikishwa mahakamani na bado shauri
hilo bado linaendelea.
Post a Comment