Kamanda wa polisi
mkoa wa Singida Linus Sinzumwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo
kwenye picha) ya wanafamilia wanne kufariki dunia baada ya kuangukiwa na nyumba
ya Tembe.(Picha na Nathaniel Limuu .
Watu wanne wa familia moja
wakazi wa kijiji cha Kilunda tarafa ya Nduguti wilaya ya Mkalama mkoani Singida
wamefariki dunia papo hapo baada ya kuangukiwa na nyumba yao ya
tembe.
Mvua nyingi zinazoendelea
kunyesha mkoani Singida hivi sasa, zimepelekea paa la nyumba hiyo ya tembe
iliyokuwa imeezekwa kwa miti aina ya mapawa na kukandikwa kwa udongo mwingi,
kuporomoka na kuwafunika wanafamilia hiyo.
Baada ya kufunikwa, miti
iliyokuwa imetumiwa kuezekea tembe hilo ilishika moto uliokuwa umewashwa kwa
ajili ya familia hiyo kukabiliana na baridi ya usiku na kuanza kuteketeza miili
ya watu hao.
Kamanda wa jeshi la polisi
mkoani Singida Linus Sinzumwa aliwataja wanafamilia hao kuwa ni Enock Edson
(22), Kefasi Edson (14), Kulwa Edson (12) mwanafunzi wa darasa la sita shule ya
msingi Nduguti, Elisha Edson (9) mwanafunzi wa darasa la tatu shule ya msingi
Nduguti.
Amesema tukio hilo la
kusikitisha limetokea mkesha wa kumakia mwaka mpya 2013 usiku wa manane wakati
familia hiyo ikiwa imelala.
Sinzumwa amesema mbali na
wanafamilia hiyo pia ndama wawili na mbuzi 1 ,walikufa kutokana na kuangukiwa na
paa la tembe hilo.
Kamanda Sinzumwa ametumia
fursa hiyo kuwataka watu wanaomiliki nyumba za tembe pamoja na kuezekwa kwa bati
wajenge tabia ya kukagua nyumba zao mara kwa mara ili kuepusha majanga au watu
kupoteza uhai na mali zao.
Post a Comment