Waziri Mkuu Mizengo Pinda akitaka maelezo zaidi kuhusu
aina ya mbegu ya mahindi iliyotumika kutoka kwa Bi. Grace Hokororo ambaye ni
Bibishamba wa kata ya Itenka wakati alipokuwa akikagua shamba darasa
analolisimamia kwenye kijiji cha Itenka wilayani Mlele, Katavi, jana jioni
(Januari 6, 2013). Alifurahia kazi yake na kuahidi kumpatia pikipiki imsaidie
kutembelea vijijiji vingine vinne anavyovisimamia. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Bibishamba wa kata ya Itenka, Bi. Grace Hokororo
akipokea zawadi ya sh. 305,000/- kutoka kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambazo
zilichangwa papo hapo na watu alioandamana nao ili kumpongeza kwa kazi nzuri
aliyoifanya kwenye shamba darasa. Wa pili kulia ni Bw. Joseph Laurent
anayesimamiwa na bibishamba huyo ambaye shamba lake lilikaguliwa na Waziri Mkuu
katika kijiji cha Itenka jana jioni (Januari 6, 2013) wilayani Mlele, Katavi.
Pia aliahidiwa kupatiwa pikipiki ili imsaidie kutembelea vijijiji vingine vinne
anavyovisimamia. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Amsifu kumkuta akiwa amevaa
unifomu, asifia shamba darasa analolisimamia
*Achangiwa sh. 505,000/ za
papo hapo
*Wanakijiji walitaka
kumtosa wakidai hawamjui
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda
amekunwa na utendaji kazi wa Bibi Shamba wa kata ya Itenka, Bi Grace Hokororo na
kuamua kumpa zawadi ya pikipiki ili imsaidie kuzungukia vijiji
anavyovihudumia.
Waziri Mkuu alitoa ahadi
hiyo jana jioni (Jumapili, Januari 6, 2013) mara baada ya kukagua shamba la
mfano katika kijiji cha Itenka B, kata ya Itenka, wilayani Mlele, mkoani Katavi.
Kabla ya hapo, Waziri Mkuu alihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya
shule ya msingi ya Itenka B.
Kabla ya kuamua kukagua
shamba darasa la mkulima anayesimamiwa na Bibi shamba huyo, Bw. Joseph Laurent,
wakiwa kwenye mkutano wa hadhara, wakazi wa kata hiyo walitaka kumtosa bibi
shamba huyo kwa kudai kwamba hawamjui na hawajawahi kuona shamba darasa
lolote.
Sekeseke lilianza wakati
Waziri Mkuu alipokuwa akisisitiza matumizi ya kilimo cha sesa na kuhoji kama
wakazi hao wanaye bwanashamba, ndipo walipojibu hawana. Bi. Hokororo
alipojitokeza wakadai hawamjui, alipoulizwa na Waziri Mkuu kama ana ushahidi
wowote, Bi. Hokororo akataja vijiji anavyovisimamia ambavyo ni Itenka “A”,
Itenka “B”, Diripu, Tumaini na Tukoma.
Bi. Hokororo (26) ambaye
amefanya kazi kwenye kata hiyo kwa mwaka mmoja na hana usafiri, aliokolewa na
wakulima wachache ambao walijitokeza na kukiri kuwa wamefundishwa kilimo bora
kwenye mashamba yao na kusimamiwa na bibi shamba huyo.
Ndipo Waziri Mkuu
alipomchagua Bw. Laurent na kumuuliza shamba lake liko wapi. “Liko hapa hapa
kijijini, amenisadia na sasa hivi ninavuna magunia 30 kwa ekari moja” alijibu
Bw. Laurent mwenye ekari tatu na kumfanya Waziri Mkuu aamue kwenda
kulikagua.
Akiwa shambani hapo,
alishangaa kukuta mahindi yamepandwa kwa mistari, yamepaliliwa vizuri na
yamewekewa mbolea naye bila kuamini alichokiona, huko huko shambani, akaahidi
kumpatia pikipiki ili imsaidie katika kazi zake.
“Kwanza huyu ni bibi shamba
wa kwanza kumkuta akiwa na unifomu… shamba zuri, limepandwa kisasa kabisa,
mahindi yamepaliliwa na tena yana mbolea. Ni mazuri kabisa! Nitampatia pikipiki
mara moja,” alisema Waziri Mkuu ambaye alikuwa anamalizia ziara yake ya jimbo
kwenye kata mbili kati ya 14 zilizobakia wakati wa ziara yake Desemba, mwaka
jana.
Kabla ya kutoka katika
shamba hilo, mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda alikusanya michango ya papo hapo
ikiwa ni zawadi kwa bibi shamba huyo na kufanikiwa kukusanya sh. 305,000/-
zikiwa ni fedha taslimu ambazo alimkabidhi hapo hapo shambani. Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, Bw. Estomih Chang’a aliahidi
kumpatia sh. 200,000/- kabla ya mwisho wa wiki hii.


Post a Comment