ZURICH,
Uswisi
SHIRIKISHO la Kimaifa la
Mpira wa Miguu (FIFA) limeahirisha uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kutokana na mkanganyiko uliojitokeza katika mchakato wa uchaguzi
huo.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga
amesema FIFA imetuma barua ikiagiza mchakato wa uchaguzi usimame baada ya kupata
malalamiko.
Amesema kutokana na
mkanganyiko huo, FIFA katika barua yake ya leo (Februari 19 mwaka
huu- imeambatanishwa) imeagiza mkutano wa uchaguzi wa TFF ambao awali
ulipangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu uahirishwe hadi hapo itakapotuma
ujumbe wake nchini.
Ujumbe huo wa FIFA
unatarajiwa kufika nchini katikati ya mwezi ujao (Machi) ambapo utafanya
tathimini ya hali hivyo, kutuma ripoti yake katika shirikisho hilo na baadaye
kutoa mwongozo wa nini kifanyike.
Rais Tenga amewaomba radhi
wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa usumbufu uliojitokeza kutokana na uamuzi huo
wa FIFA, hivyo kwa sasa hakutakuwa tena na mkutano huo mpaka hapo watakapopewa
taarifa nyingi.
Amesema TFF inakaribisha kwa
mikono miwili uamuzi huo wa FIFA kwa sababu ni chombo ambacho cha juu kimpira
duniani, na hatua hiyo ina lengo la kuhakikisha kuwa kila mhusika katika
mchakato huo wa uchaguzi anapata haki yake.
“Nia yetu ni kuona watu
wanatendewa haki, na nia ya FIFA ni kutafuta ukweli. Hivyo wahusika (waathirika)
wajiandae, watumie wakati huu kuandaa hoja zao ili FIFA wakifika wawasikilize,
wapate maelezo ya kina kuhusu utaratibu na malalamiko yaliyotolewa,” alisema
Tenga.
Rais Tenga amesema timu hiyo
ya FIFA itakapofika yenyewe ndiyo itakayopanga izungumze na nani kwa wakati
gani, hivyo ni vizuri waathirika na vyombo vyote vilivyohusika na mchakato wa
uchaguzi wakajiandaa.
Amesema ilikuwa ni muhimu
suala hili likatatuliwa katika ngazi ya FIFA kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi
utakapofanyika TFF inaendelea kuwa chombo kimoja badala ya kurudi katika
migogoro iliyokuwepo huko nyuma.
“Nataka tubakie kama
tulivyokuwa. Malumbano yaishe. Pangeni hoja, wakija hao waheshimiwa (FIFA)
muwaambie. FIFA ni chombo cha juu, nafurahi wamekubali kuingia katika hili,
kwani wana shughuli nyingi wangeweza kukataa,” amesema.
Kuhusu fursa ya kufanya
marejeo (review) kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi inayoongozwa na Idd
Mtiginjola ambayo aliielezea Jumamosi, Rais Tenga amesema kwa vile hicho ndicho
chombo cha mwisho nchini katika masuala ya uchaguzi alishauriwa kuwa kingeweza
kufanya review.
“Kwa vile hakuna chombo
kingine, nikashauriwa kuwa kinaweza kufanya review. Katika utaratibu wa kutoa
haki, uamuzi ni lazima uwe wa wazi kwa kutoa sababu. Nilidhani hilo
linawezekana, kwani Mahakama Kuu hufanya hivyo. Kwa hili uamuzi wa Mtiginjola ni
sahihi,” amesema Rais Tenga.
Kamati ya Mtiginjola
iliyokutana jana (Februari 18 mwaka huu) ilitupa maombi ya review
yaliyowasilishwa mbele yake na waombaji uongozi watano kwa vile hakuna kipengele
chochote kwenye Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi kinachotoa fursa
hiyo.
Waombaji hao walikuwa Jamal
Emil Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa TFF na Hamad Yahya aliyeondolewa
kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL
Board).
Wengine ni walioomba kuwania
ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Kanda zao kwenye mabano; Eliud Peter
Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi (Morogoro na Pwani) na Mbasha Matutu
(Shinyanga na Simiyu).
Post a Comment