Imeripotiwa kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, amepokea
jumbe za maneno 400 na za miito ya simu 200 zenye matusi ya nguoni kutoka kwa
watu wakimtaka ajiuzulu. Mtoa habari wa HabariLeo ambaye yupo karibu na Spika
Makinda amesemea jumbe hizo zimerekodiwa.
Kwamba, Spika alianza kupokea jumbe hizo kuanzia juzi,
baada ya viongozi wa CHADEMA kutangaza namba za simu za Spika kwenye mkutano wa
hadhara na kuendelea jana ili kutumia ‘nguvu ya umma’, kumlazimisha
ajiuzulu.
Sababu ya kutumwa jumbe hizo inaripotiwa kuwa ni baada
ya hatua ya Spika Makinda kutangaza mabadiliko ya Kamati za Bunge, yaliyoivunja
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na shughuli zake kuwekwa
chini ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) ambapo katika mabadiliko hayo,
aliyekuwa Mwenyekiti wa POAC, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
hakuridhishwa nayo na hivyo kumshitaki Spika Makinda kwa Wananchi ili
wamng’oe.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah, alipozungumza
na gazeti hili juzi, alisema uamuzi huo haukufanywa na Spika Makinda peke yake,
bali ni baada ya kushauriana na Kamati ya Kanuni za Bunge, ambayo iliridhika na
sababu za kuchukuliwa uamuzi huo.
Wajumbe wa Kamati iliyoridhia makubaliano hayo mbali na
Spika na Naibu Spika, ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA). Wengine ni Mbunge wa Mbulu, Mustapha
Akunaay (CHADEMA), Mbunge wa Kibondo, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), Mbunge wa
Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF) na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed
(CUF). Pia Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM), Mbunge wa Bariadi
Magharibi, Andrew Chenge (CCM), Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani (CCM),
Mbunge wa Viti Maalumu, Pindi Chana (CCM) na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod
Mkono (CCM).
Dk Kashilillah alisema mabadiliko hayo hayakuigusa
kamati ya POAC peke yake, bali kamati zingine kama ya Sheria Ndogo na ya Ulinzi,
Usalama na Mambo ya Nje, ambayo imegawanywa mara mbili.
Akielezea sababu za kuvunja POAC, Dk Kashilillah
alisema lengo lilikuwa ni kuunganisha wizara, taasisi zake na mashirika yaliyo
chini ya wizara husika, ili yawe na msemaji mmoja.
Alisema awali Waziri alikuwa anawajibika PAC, wakati
mashirika ya umma yaliyo chini ya wizara yakiwajibika chini ya POAC. Kwa mujibu
wa Dk Kashilillah, kulikuwa na mkanganyiko mkubwa na akaeleza kuwa hatua ya
kuunganisha wizara na mashirika yake ya umma, kutafanya sasa Waziri, Katibu
Mkuu, Mwenyekiti wa Bodi na watendaji wakuu wa mashirika, kuwajibika kwa kamati
moja ya PAC. Dk Kashilillah alisema sababu nyingine ni kuangalia utendaji katika
baadhi ya nchi, ambazo alisisitiza kuwa hazina kamati za mashirika ya
umma.
Mwandishi aliwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA), ambayo iliweka wazi kuwa hakuna sheria yoyote inayozuia mtu
kutoa namba ya simu ya mwingine kwa mtu au watu wengine, bila ridhaa ya mwenye
namba ya simu. Ofisa wa TCRA, ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu si
msemaji wa taasisi hiyo, alisema sheria ya kuzuia utoaji namba na taarifa za mtu
mwingine, inakataza kampuni za simu kufanya hivyo, lakini haizungumzi kwa mtu
binafsi. Ofisa huyo alinukuu sheria hiyo:
Taarifa ni siri ya mtu husika, isipokuwa kama mtu
huyo ameitoa kwa ridhaa yake.
Alisema pamoja na kuwapo na kipengele hicho, mtu yeyote
ambaye ana namba ya simu ya mtu mwingine, hazuiwi kutoa namba hiyo kwa watu
wengine.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, wamesema ingawa namba za simu za viongozi
hao zinaweza zikapatikana kwa kila mtu, kuzigawa katika mkutano huo ambao
ulikuwa na mtazamo hasi kwa Spika na Naibu wake, kulikuwa na nia
mbaya.
Kama ungekuwa mkutano au semina yenye nia njema na
Spika, ungesema wamegawa simu kwa nia njema. Lakini mkutano huo ulivyokuwa na
kauli mbovu kwa Spika na taasisi ya Bunge, kitendo cha kuwapa watu namba
kinamaanisha walitaka hao watu wamtukane pia. katika mkutano kama huo, kunakuwa
na watu wa kila aina wakiwamo wasio na busara.
Hivyo viongozi hao wa CHADEMA waliofanya hivyo,
wameshindwa kutumia busara. Mjumbe wa NEC, Juma Killimbah, ambaye aliwahi kuwa
Mbunge na kuhadharisha wananchi wasije kujikuta katika mkono wa sheria kwa
kutumia namba hizo vibaya kwa kutoa matusi, alisema simu ya kiongozi huyo
kujulikana si ajabu na ni jambo la kawaida.
Source: http://www.wavuti.com
Post a Comment