Ndugu zangu,
Kwenye
vyombo vya habari juma hili, moja ya habari kubwa iliyochagizwa sana ni
kitendo ch viongozi wa Chadema kutoa kwa wananchi, pale viwanja vya
Mwembe Yanga, namba za simu ya mkononi ya Spika Anne Makinda na Naibu
wake, Job Ndugai.
Kimsingi,
viongozi wa Chadema waliofanya kitendo kile walikosea. Yawezekana
kabisa kuwa madai ya Chadema kuwa Spika na Naibu wake wanaisiginya
demokrasia ndani ya Bunge ni madai ya msingi, lakini, namna waliyochagua
ya kufikisha madai hayo kwa wananchi haikuwa sahihi.
Ni
kawaida, kwa baadhi ya viongozi wawapo majukwaani kusukumwa na jazba
wanapoongea, lakini, hutokea pia, kauli za viongozi hao wawapo
majukwaani zinapokosa umakini, kupelekea madhara makubwa.
Katika
kazi yangu ya uandishi, nimeshawahi kutofautiana na Spika Makinda, si
mara moja, mara ya mwisho ni kwenye hoja yake kuwa wabunge wawapo Dodoma
wana maisha magumu, hivyo, kuhalalisha ongezeko la posho zao.
Lakini
bado naamini, Spika Makinda ni binadamu kama wengine. Naye ni mzazi na
mwenye familia yake inayomzunguka. Kitendo cha viongozi wa Chadema kutoa
hadharani namba za Spika Makinda , za simu ya mkononi, kwenye umati wa
watu wenye kero mbali mbali , na unaoambiwa kuwa watumie namba hizo
kumpigia na kutuma ujumbe mfupi kwa Spika Makinda, bila shaka, kwa akili
ya kawaida tu, kitapelekea Spika Makinda na mwenzake Ndugai kuwa na
wakati mgumu. Maana, watu wale watakuwa wamechochewa.
Ikumbukwe,
kijinsia Anne Makinda anaweza kuwa mhanga zaidi wa kupigiwa na kutumiwa
jumbe za simu zenye hata kumdhalilisha kijinsia. Katika dunia hii kuna
baadhi ya wanaume wenye maradhi ya kisaikolojia yenye kuhusihanisha
masuala ya ngono.
Kwamba
kuna wanaume ambao hutafuta namba za simu za wanawake tu. Ikifika usiku,
hupiga bila kuongea, wanachosubiri ni kusikia sauti ya mwananmke
ikijibu na kisha kumaliza haja zao. Hao ni wagonjwa. Hivyo, unapotoa
hadharani namba ya simu ya mkononi ya mwanamke, basi, unaweza pia
kumuingiza katika hatari ya kupokea simu za ajabu ajabu kutoka kwa
baadhi ya wanaume. Wako wapi wanaharakati wa haki za kibinadamu na
kijinsia wa kumtetea Anne Makinda?
Tunajifunza nini?
Viongozi
wa kisiasa wawe makini wawapo majukwaani. Mambo mengine wanaweza
kuyafanya na hata kuyaongea majukwaani wakidhani kuwa wameyafanya kwa
dhamira njema, lakini, matokeo yake yaweza kuwa na madhara makubwa.
Ingewezekana
kabisa kwa viongozi wale wa Chadema kutoa hadharani namba maalum ya
simu ya mkononi, ili watu wapige na watume jumbe fupi kwenye simu hiyo.
Kisha, viongozi hao wangeweza kurekodi sauti zenye maoni ya watu yasiyo
na matusi wala namna yoyote ya kudhalilisha. Wangekusanya pia jumbe hizo
fupi kwa kuhariri zile zenye matusi na zenye kudhalilisha. Baadae
zingewakilishwa kwa Spika Makinda na Naibu wake.
Ingewezekana
pia kukusanya saini kutoka kwa wananchi zenye kuonyesha kuwa
wanawapinga Spika na Naibu wake, na kwamba wanawashinikiza wang'oke.
Hizi zote ni njia za kistaarabu kabisa za kuwasilisha malalamiko.
Tukishindwa
kuonyesha mfano sasa, wa kufuata taratibu za kistaarabu, hatari yake
tunaizoesha jamii kutumia njia za ovyo na nyingine zenye maovu katika
kuwasilisha malalamiko yao. Na kesho huenda Spika wa Bunge atatoka
Chadema.
Itakuwaje
basi, pale kesho viongozi wa CCM nao watasimama Mwembe Yanga mbele ya
wananchi wenye kero zao, na kutaja namba za simu ya mkononi za Spika wa
Bunge linaloongozwa na Chadema?!
Hapana, hivi tunavyoenenda sivyo inavyopaswa twende. Na hakuna aliyekamilika. Tujisahihishe.a
Maggid Mjengwa,
Post a Comment