Katika siku za hivi karibuni,
kumetokea matukio ya ukatilii dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi
ambayo yaliriripotiwa na vyombo vya habari likiwemo tukio lililotokea
katika kitongoji cha Kivifuti, Sumbawanga mkoani Rukwa ambapo gazeti la
Habari LEO la tarehe 13 Februari, 2013, liliripoti kuwa, Bi. Maria
Chambanege (39) mwenye ulemavu wa ngozi alikatwa mkono. Halikadhalika,
katika magazeti ya JAMBO LEO na MTANZANIA ya tarehe 17 /2/2013,
yameripoti tukio kama hilo kutokea mjini Sumbawanga ambapo mtoto
Mwigula Magessa (7) mwenye ulemavu wa ngozi nae alikatwa mkono na watu
wasiojulikana na kutokomea nao.
Kutokana na ukatili waliofanyiwa
wakazi hao wenye ulemavu wa ngozi, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia
na Watoto inakemea na kulaani vikali matukio hayo ya ukatili ambayo
yanawanyima watu wenye ulemavu wa ngozi haki yao ya kuishi kwa amani na
utulivu kama ilivyo kwa wananchi wengine. Wizara inamtaka kila
mwanajamii kulinda na kuthamini uhai wa mtu mwingine ikiwemo kuheshimu
sheria na haki za binadamu.
Ikumbukwe kuwa, vitendo hivyo vya kikatili
siyo tu vinaathiri aliyefanyiwa ukatili, bali pia vinagusa na kuathiri
maisha ya watu wengine katika jamii; na kuchafua sifa ya nchi yetu.
Aidha, Wizara inaitaka jamii
kubadilika na kuachana na imani potofu ambazo zinahatarisha maisha na
usalama wa watu wengine na ambazo zinarudisha nyuma jitihada za Serikali
za kupiga vita ukatili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, wanawake na
watoto. Wizara inawataka wananchi wote, kuwafichua wale wote
wanaojishughulisha na vitendo hivyo na kutoa taarifa kwa walinzi wa
amani katika maeneo yao ili Serikali iweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu
wa sheria.
Kwa matukio hayo, na mengine
ambayo yameripotiwa na vyombo mbalimbali likiwemo la utupaji wa watoto
wachanga matukio ambayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Iringa, Michael Kamhanda na kuripotiwa na gazeti la MTANZANI la tarehe
13 Februari, 2013. Tukio lingine ni la mtoto Kaselemako Mpale (14)
aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Kasumulu Wilayani Kyela Mkoani
Mbeya ambaye alichinjwa na baba yake mzazi Mpale Mbisa (35) kutokana na
imani za kishirikina. Aidha, kijana Malba Hamisi(19) wa Wilaya ya
Kishapu anayetuhumia kumuua bibi yake Mindi Dotto (70) kwa imani za
kishirikina.
Kutokana na taarifa hizo za
ukatili ambazo zimeripotiwa na vyombo vya habari, Wizara inapenda
kupongeza jitihada zilizofanywa na vyombo vya habari vyote ambavyo
vimekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha na kuripoti matukio
mbalimbali ya ukatili unaofanyika katika jamii jambo ambalo limeisaidia
Serikali kubaini na kufuatilia taarifa za ukatili mara vitendo hivyo
vinapotokea. Aidha, ripoti hizo zimesaidia kuamsha ari kwa wananchi
kuripoti matukio ya ukatili mara zinapotokea, jambo ambalo limesaidia
kuwachukuliwa hatua za kisheria wale wote wanaobainika kuhusika na
matukio hayo. Wizara inahimiza wananchi kuendelea kufanyakazi kwa juhudi
na maarifa na kupuuza imani za ushirikina katika kujiletea maendeleo
yao.
Erasto T. Ching’oro
Msemaji wa Wizara
Post a Comment