ASKARI Polisi PC Yohana mwenye namba 7771 amemuua kwa kumpiga risasi
mwendesha bodaboda, Makisio Ngonyani (27), kisha naye akauawa na watu wenye
hasira kwa kutumia mawe na mbao.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea jana katika eneo la Ngwinde wilayani
Namtumbo mkoani Ruvuma.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, lilitokea majira ya saa 8 mchana jana
ambapo PC Yohana na mwenzake PC Venance Kamugisha wa kituo kikuu cha polisi cha
wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, walikuwa katika doria ya kawaida.
Walipofika katika Kijiji cha Litola na kupata chakula cha mchana kwenye moja
ya migahawa iliyopo hapo, walianza kazi ya doria ya kawaida ambapo alitokea
mwendesha bodaboda huyo akiwa amebeba abiria wawili kinyume na sheria ya usalama
barabarani na walipomsimamisha, hakutii amri hiyo huku kundi jingine la
waendesha bodaboda likiwazuia askari hao kufanya kazi yao.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, hali hiyo ilimfanya PC Yohana kufyatua risasi
iliyompata mmoja wa abiria kwenye kidole cha mkono na kisha kupitiliza na
kumpiga Ngonyani kichwani na kusababisha kifo chake papo hapo.
Baada ya tukio hilo, askari hao walikimbia na pikipiki waliyokuwa nayo, huku
wakifukuzwa na kundi la waendesha bodaboda wengine hadi katika Kijiji cha
Ngwinde ambapo waliwazingira na kumpiga kwa mawe PC Yohana na kumsababishia kifo
huku wakimjeruhi PC Kamugisha ambaye alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa wa
Ruvuma mjini Songea.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma,
Deusdedit Nsimeki aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu akiwa eneo la tukio
kwamba askari huyo aliuawa kwa kutumia mawe na mbao.
TANZANIA DAIMA
Loading...
Post a Comment