SHY - ROSE |
Shy-Rose alisema hayo jana akijibu kauli ya Waziri Sitta kwamba baadhi ya wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), akiwemo yeye hawahudhurii vikao vinavyoitishwa na wizara hiyo na kwamba wamekuwa wakidai posho.
Akijibu kauli hiyo kwa maneno makali, Shy-Rose alimtaka Waziri Sitta na naibu wake kutoa vielelezo dhidi ya madai yao.
“Kama nilivyosema kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wizara imejitenga sana katika kutoa mwongozo na vile vile katika kuwafikia Watanzania walio wengi kwa kigezo kwamba haina fedha.
“Nimekuwa nikiwasiliana moja kwa moja na Naibu Waziri Abdullah Juma Sadallah kuhusu masuala mengi kwa maana ya kushirikiana na kupeana mwongozo, lakini majibu ya Naibu Waziri daima yamekuwa ni ya ubabaishaji na ya kukatisha tamaa, akisema kwamba wabunge wa EALA hawako chini ya wizara,” alisema Shy-Rose.
Mbunge huyo amemtaka Waziri Sitta kukaa na viongozi wa wizara yake ili apate ukweli wa mambo kuliko kurukia kujibu hoja kwa ubabaishaji kwani nia ni kuweka maslahi ya nchi mbele na si binafsi kama alivyofanya juzi yeye na naibu wake kwenye kikao cha kamati.
“Kwa vile amenitaja mimi moja kwa moja kuwa ni kinara wa kutoa udhuru… nasema si kweli hata kidogo… ninamheshimu Waziri Sitta kama kiongozi na kama mzazi wangu, lakini kauli yake imenisikitisha sana sana kwani amenifedhehesha kwenye jamii kwa kutoa kauli za kunichafulia jina langu kwa vile nimesema ukweli.
“Ni Waziri Sitta huyo huyo kwenye kikao cha bajeti mwaka jana bungeni Dodoma nilikuwa miongoni mwa wabunge aliowapongeza kwa kazi nzuri. Leo iweje abadili kauli yake? Au ni kwa vile nimesema ukweli?” anahoji Shy-Rose na kuongeza kuwa penye ukweli hatasita kuwaumbua viongozi ambao hawawajibiki.
Kuhusu suala la posho, alisema walialikwa mara moja tu bungeni lakini waliambiwa kila mtu ajigharamie malazi na usafiri.
“Hivi inaingia akilini kweli ualikwe kwenda safari halafu unaambiwa ujigharamie? Yeye Sitta na Naibu Waziri kwa vile wanatumia magari ya wizara na kuwekewa mafuta na kupewa posho kufika bungeni ndiyo maana inamwia rahisi kuongea kiubabaishaji.
“Licha ya wizara kukataa kutugharimia, lakini nilikuwa miongoni mwa wabunge waliohudhuria kikao cha bajeti ya wizara huko Dodoma… hiki ni kielelezo tosha kabisa suala la posho ni agenda ya uongo ili wizara kujisafisha kwenye kamati na Watanzania kwa ujumla.
“Hivi inaingia akilini kweli eti tunadai posho kuhudhuria vikao vya kupewa mwongozo tena hapa Dar?” anahoji Shy-Rose na kuongeza kuwa suala la posho kwake binafsi halijawahi kuwa agenda kuu hata siku moja.
“Hii hoja ya posho si ya kweli hata kidogo, kilichoongelewa ni vipi tunafika Dodoma iwapo hatujui tutalala wapi na tutakula nini. Sijaomba gharama hizi kama Shy-Rose bali kama Katibu wa Wabunge wa EALA,” aliongeza.
Shy-Rose alisema ni jambo la kusikitisha kwamba Watanzania walio wengi hawaifahamu Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa upana wake, hivyo juhudi za ziada zinahitajika kwa wizara kushirikiana na wabunge wa EALA ili kuwafikia Watanzania wengi kufahamu mtengamano huu.
Mbunge huyo alisema semina pekee iliyowahi kufanyika kwa wabunge wa EALA ilikuwa mara baada ya kuchaguliwa takriban miezi kumi iliyopita.
Katika semina hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na wizara, waliambiwa wizara itakuwa inatoa mwongozo kabla ya vikao vya Bunge kuanza ili kuweka maslahi ya taifa mbele na baada ya hapo hawajawahi kuitwa tena na wizara hiyo.
Kwa mujibu wa Shy-Rose, kikao pekee kilichoitishwa na wizara ni Januari mwaka huu jijini Bujumbura wakati ambapo mbunge huyo alikuwa nchini India kwa matibabu.
Juzi wakati Waziri Sitta akitoa ufafanuzi katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Waziri Sitta alisema madai ya wabunge wa jumuiya hiyo kwamba hawashirikishwi katika vikao vya wizara yake sio ya kweli kwani wengi ni mabingwa wa kutoa udhuru na wanataka posho.
TANZANIA DAIMA
Post a Comment