Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Wanafunzi wa Udaktari wanaosomeshwa chini ya Mabingwa kutoka Jamuhuri ya Watu wa Cuba ambao wanatarajiwa kumaliza mafunzo yao miaka sita fikapo mwezi Julai mwaka huu wa 2013.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akibadilishana mawazo na Mabingwa kutoka cuba wanaotoa mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari 50 kutoka Zanzibar hapo Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Saleh Mohammed Jidawi akisisitiza jambo mara baada ya mkutano wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Wanafunzi wa Udaktari hapo Mnazi Mmoja Hospitali.(Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ).
Na. Othman Khamis Ame- Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewakumbusha Madaktari Nchini kuzingatia maadili yao ya kazi kama wanavyokula kiapo lengo likiwa kuwapa faraja na afuweni wagonjwa wanaokwenda Hospitalini na Vituo vya afya ili kupata huduma bora za afya.
Kumbusho hilo alilitoa wakati alipowatembelea na kuzungumza nao Wanafunzi wa Fani ya Udaktari wanaopata mafunzo chini ya Madaktari mabingwa kutoka Jamuhuri ya Watu wa Cuba hapo Hospitali kuu ya Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.
Balozi Seif amesema Wagonjwa na hasa Wananchi hujenga matumaini mazuri wakati wanapopata huduma safi, na hii hupatikana iwapo madaktari husika watakuwa wakizingatia zaidi taratibu zinazowaelekeza kutekeleza vyema majukumu yao ya kila siku.
Amesema Serikali imelazimika kuwa na utaratibu maalum wa kuwasomesha vijana wake katika fani ya Udaktari hapa Nchini kwa matumaini ya kuwa na watendaji wa kutosha wa sekta hiyo watakaokidhi mahitaji hapa Nchini.
“ Utafiti unaonyesha kwamba utaratibu huu umeonyesha mwanga wa kupata idadi kubwa ya madaktari wazalendo mpango ambao unapunguza wimbi la ukimbizi kwa vijana wetu wanaopata fursa ya kusoma vyuo vya nje, akavitolea mfano vile vya ulaya na Bara la Asia kwamba wakimaliza mafunzo yao wanaishia katika Nchi hizo kimaisha”. Alifafanua Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba mpango huu ulionzishwa kwa karibu miaka sita iliyopita ni mwanzo mzuri kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzisha mafunzo ya Sayansi ya Udaktari katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA }.
Aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha kwamba lile lengo lililokusidiwa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ya kuwa na Madaktari zaidi wazalendo Nchini wanalitekeleza vyema kwa kufanya kazi kwa bidii mara wamalizapo mafunzo yao.
Balozi Seif alielezea matumaini yake kwamba wanafunzi hao watatekeleza majukumu yao wakielewa kwamba watu wanaowahudumia ni miongoni mwa ngugu, wazee na jamaa zao waliowazunguuka.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza walimu wa wanafunzi hao Kutoka Jamuhuri ya Watu wa Cuba kwa umahiri wao wa kusaidia kuwafinyanga vyema wanafunzi hao wa fani ya Udaktari Zanzibar.
Mapema wakielezea changamoto zinazowakabili chuoni hapo baadhi ya Wanafunzi hao walisema ufinyu wa posho sambamba na ucheleweshwaji wake ni moja ya tatizo lililokuwa likiwapa usumbufu mkubwa wakati katika mafunzo yao.
Walizitaja changamoto nyengine kuwa ni pamoja na kupatiwa fursa za masomo ya juu hapo baadaye iwe ndani au nje ya Nchi pamoja na migongano baina yao na baadhi ya wafanyakazi wa Hospitali Kuu ya Mnazi mmoja wakati wanapokuwa katika mazoezi ya vitendo.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hizo Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Saleh Mohammed Jidawi alisema asilimia kubwa ya changamoto hizo zimo ndani ya uwezo wa Wizara husika ambapo aliwawakikishia kwamba Uongozi wa Wizara utazifanyia kazi kadri hali inavyoruhusu.
Dr. Jidawi alisema ni fahari kwa Uongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Afya kuona kwamba Wanafunzi hao wanafanikiwa vyema katika maisha yao ya kazi hapo baadae kwani kwa mujibu wa fani yao wao ni miongoni mwa sehemu ya Wizara hiyo.
Wanafunzi hao 50 ambao kati yao 38 kutoka Unguja na 21 kutoka Kisiwani Pemba wanatarajiwa kumaliza mafunzo yao ya miaka Sita ya Udaktari katika daraja la Udaktari { yaani Medical Doctor – M.D } ifikapo mwezi Julai mwaka huu wa 2013.
Post a Comment