Ndugu zangu, habari za
mapumziko ya mwisho wa wiki. Yapo mambo machache ningependa kuwashirikisha ili
kuweka kumbukumbu sawa, na pia kuzuia upotoshaji ambao unaweza kujitokeza siku
za usoni iwe kwangu, kwako au kwa mtu mwingine.
Mojawapo ya mambo makubwa ambayo yamejitokeza siku za
karibuni hasa katika suala la Teknolojia na habari
ni jambo la sheria za faragha (privacy and privacy laws). Tumeshuhudia kufungwa
kwa gazeti za News of The World mali ya bilionea Rupert Murdoch wa Kimarekani
baada ya kudhihirika alitumia wataalam wa teknolojia (hackers) kutafuta siri za
watu mashuhuri kwa kuingia katika simu zao za mkononi kinyume cha utaratibu na
sheria za faragha (Privacy Laws). Tumeshuhudia pia wahalifu hao hao wa mtandao
wakifanya mengi kama kuvamia kwa mitandao ya makampuni makubwa kama Sony na
mengineyo na hata katika mitandao hii ya kijamii upo wakati marafiki zako
wanakwambia mbona umenitumia kitu kisichoeleweka, na baadaye kuja kugundua
kwamba si wewe uliyefanya hivyo.
Tarehe 1, 8 na
9 mwezi huu wa Machi nilikuwa Dar es Salaam kwa shughuli zangu za kawaida
kimaisha lakini ziko updates 5 zilifanyika hapa moja ikimhusu ndugu Absalom
Kibanda. Ni ajabu kwamba baadhi ya waandishi tena waliojivika taji la usahihi
katika uandishi waliiandika habari hiyo bila hata kuniuliza kwamba ni nini
kinatokea. Tunajitahitahidi na kutamani kuwa na Taifa la waandishi makini na
wenye kufuata maadili lakini wapo wanaoturudisha nyuma. Ni ajabu gazeti kuandika
jambo lisilo la kweli huku wahusika wakiwa na kila uwezo wa kumfikia yule
wanayedhani kwamba ameandika na kumhoji ili kuhakiki habari. Kazi ya uhariri ni
kuhakiki. Ikiwa mtu atakimbilia kuandika jambo likuhusulo ambalo hana hakika
nalo na alikuwa na kila uwezo wa kuwasiliana na wewe na kukuuliza lazima
utajiuliza maswali mengi. Kwanza, nini hasa lengo lake? Pili, ufahamu wake wa
kile anachokifanya kwa maana ya taaluma yake katika kazi
anayoifanya.
Napenda
kuwaambia kwamba katika tarehe hizo mwezi huu wa Machi, wahalifu wa mtandao
wakiwa eneo la Njiro na baadaye Kijenge mjini Arusha, kila post ilionyesha eneo
ilipotoka, (wakati huo mimi nikiwa Dar es Salaam) waliingia bila idhini kwa njia
haramu (Hacking) katika anuani yangu ya Facebook na ku-post habari hizo tano.
Sasa nimeliacha jambo hilo katika vyombo stahiki vya ulinzi na usalama ili
kufuatiliwa kadiri ya taratibu zao.
Natoa wito kwa
ndugu zangu waandishi kujitahidi kuhakiki habari kabla ya kuzipeleka katika
vyombo vyao na pia wahariri kuzingatia kuhakiki habari kabla ya kuzichapisha
hasa kama chombo chako cha habari si cha habari za udaku. Hii itasaidia wao
kujenga heshima mbele ya jamii, kufikisha kile hasa ambacho ni habari na kuzuia
mikanganganyiko isiyo ya lazima. Haya yakizingatiwa nadhani hata sintofahamu
hizi za uandishi wa habari unaotokana na hisia na vyanzo vumbi na ufahamu mdogo
wa jambo utaondoka na tutakuwa na jamii ambayo haki na uwajibikikaji wa
wanahabari kwa jamii utaonekana kutendeka.
Niombe radhi
kwa ndugu yangu, rafiki yangu na pia mwalimu wangu, Ndugu Absalom Kibanda kwa
usumbufu wowote uliojitokeza ambao naamini watu wasio na nia njema walitaka
kuutumia kuleta hisia tofauti katika jamii na pia kumpa pole kwa mara nyingine
tena kwa maumivu yaliyosababishwa na ujangili huo. Namuombea kwa Mungu ampe
unafuu mapema zaidi ili arudi katika meza yake kuendeleze harakati za kupambana
na mchango wake katika kuleta maendeleo ya kweli kwa nchi
yetu.
Nawapa pole pia wale wote
ambao kwa namna moja au nyingine walikwazwa na uzushi huo, kwa kuwa sina tatizo
lolote na Ndugu Kibanda na wala nisingependa lililomtokea limtokee yeye wala mtu
mwingine yeyote.
Ni imani yangu ya dhati kwamba vyombo husika katika
nchi yetu havitasita kulitalifanyia kazi jambo hili na ukweli juu ya nini
kimemtokea Bwana Absalom Kibanda utajulikana na kuwekwa bayana.
Mwisho,
shukrani kwa wote mlionipigia simu kuhusu hili, tuko pamoja na nawatakia kila la
kheri katika shughuli za ujenzi wa Taifa letu hili la Tanzania ambalo msingi
wake umejengwa katika haki, umoja, amani na kujali hali za watu
wake.
Asanteni
sana.
Ndugu
yenu,
Ridhiwani
Kikwete,
Dar es Salaam,
Jumapili Machi 17,
2013.
Post a Comment