Watu
wanaoaminika kuwa ni majambazi, wamemjeruhi kwa kumpiga risasi Mtawa wa Kanisa
Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Shobana Synd na kumpora kiasi kikubwa cha
fedha.
Habari kutoka kwa
wenzake zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
zinasema kuwa mtawa huyo raia wa India kutoka Shirika la Notre Dame,
alishambuliwa kabla ya kuporwa fedha hizo.
Kwa mujibu habari hizo,
mtawa huyo aliyekuwa akitoka benki, alijeruhiwa kwa risasi mbili wakati
akisubiri kufunguliwa geti la kuingia katika Shule ya Msingi Notre
Dame.
Ingawa Watawa hao
hawakuwa tayari kutaja kiasi cha fedha zilizoporwa, habari zinasema ni zaidi ya
Sh20 milioni zilizochukuliwa benki kwa ajili ya malipo na shughuli mbalimbali za
shule hiyo.
Shule ya Msingi ya Notre
Dame iliyoko eneo la Njiro, jijini Arusha inamilikiwa na shirika hilo la Watawa
ambao wengi wao wana asili ya Asia ambako mtawa huyo, Shobana ndiye Mwalimu Mkuu
wa shule hiyo. “Alipigwa risasi mbili, moja kwenye mguu wa kushoto uliovunja
mfupa na nyingine ilipenya kwenye nyama za mkono wa kushoto ambako kwa bahati
haijagusa mfupa...Tunamshukuru Mungu anaendelea vizuri,” alisema mmoja wa watawa
kwa sharti la kutotajwa jina gazetini.
Akizungumza katika wodi
ya Hospitali ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), alikolazwa,
mtawa huyo alisema: “Ninamshukuru Mungu kwa kuninusuru katika
kifo...Walinirushia risasi kadhaa wavamizi hao.
“Ninamshukuru Mungu kwa
yote yaliyotokea, si ujanja wala uwezo wangu kuendelea kuwa hai hadi leo baada
ya mashambulizi yale ya risasi. Ninawaombea msamaha na rehema wahusika ili
waache uovu na kurejea katika njia ya haki.”
Kamanda Sabas mbali na
kukiri kutokea kwa tukio hilo alishindwa kulizungumzia kwa undani kwa maelezo
kuwa muda huo alikuwa akiendesha gari na kuahidi kulitolea ufafanuzi
leo.
Kumekuwa na matukio
kadhaa ya wateja wanaochukua fedha kutoka benki mjini Arusha kuvamiwa na kuporwa
fedha, matukio ambayo yanazua hisia ya kuwapo mtandao wa uhalifu unaoshirikisha
baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hiyo.
Mwaka jana, wafanyakazi
wawili wa Shirika la Here’s Life Africa Mission linalomilikiwa na Askofu wa
Kanisa Anglikana Dayosisi ya Mount Kilimanjaro, Stanley Hotay waliochukua fedha
katika moja ya benki hizo walivamiwa na kuporwa zaidi ya Sh10
milioni.
Tayari uongozi wa benki
zilipochukuliwa fedha hizo umeanza uchunguzi kuhusu jambo hilo kwa nia ya
kubaini kwa nini taarifa za wateja wanaochukua fedha zinafika kwa majambazi
ambao huwapora njiani au baada ya kufika ofisini kwao.
source
mwananchi
Post a Comment