Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Philipo Mulugo
Philipo Augustine Mulugo ndiyo jina lake
halisi ambalo alilisomea mpaka alipohitimu darasa la saba kwa mara ya kwanza
1988, lakini kutokana na kwamba hakufaulu kwenda sekondari alirudia darasa
hilo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa
takriban miezi mitatu sasa umebaini kuwa 1989, Mulugo alirudia darasa la saba
katika Shule ya Msingi Rukwa ya mkoani Mbeya akitumia jina la Hamimu
Hassan.
Imebainika kuwa kabla ya kuhitimu darasa la
saba kwa mara ya pili, alibadili jina hilo (kutoka Hamimu Hassan) na kuwa Hamimu
Augustino ambalo aliendelea nalo wakati akisoma elimu ya sekondari katika Shule
ya Sekondari kutwa ya Mbeya (Mbeya Day) mwaka 1990.
Hata hivyo, Mulugo mwenyewe akizungumza na
gazeti hili jijini Dar es Salaam alipuuza tuhuma hizo kwa kusema kuwa ni njama
za kisiasa zinazofanywa na maadui zake. Mulugo anasema madai hayo yamekuwa
yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti vyake halali
vya shule.
“Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui
utakuwa mtu wa 20 kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka
ushahidi nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo na kuongeza:
“Haya mambo kabla hata sijachaguliwa kuwa
Mbunge, tulivyokuwa bado kwenye mchujo wa ndani, usiku wa manane watu
walisambaza huu uvumi na nilivyoenda kwenye kikao nikatoa vyeti vyangu,
wakaviona.”
Waliomfundisha
Baadhi ya walimu waliomfundisha Mulugo, watu
waliofanya kazi naye pamoja na wakazi wa Kijiji cha Udinde alikozaliwa, maelezo
yao yanathibitisha mabadiliko ya majina ya Mulugo kwa nyakati tofauti pia ngazi
mbalimbali za kielimu.
Uchunguzi unabainisha kuwa baada ya kuhitimu
kidato cha nne, alifaulu kwenda Shule ya Sekondari ya Wavulana, Songea ambako
alisoma kati ya 1994 na 1996 akiendelea kutumia jina la Hamimu
Mulugo.
Baada ya kuhitimu kidato cha sita, uchunguzi
ulibaini kuwa Mulugo alirejea Mbeya na 1998 alilazimika kubadili tena jina pale
alipotumia cheti cha mtu aitwaye Dickson Mulungu, kuombea kazi ya kufundisha
katika Shule ya Sekondari ya Southern Highlands.
Habari zinasema Mulugo alichukua hatua hiyo
ili kumshawishi mmiliki wa shule hiyo mfanyabiashara, Gulnoor Dossa (sasa ni
marehemu), kumpa nafasi ya kufundisha shuleni hapo.
“Mulugo alilazimika kutumia cheti cha rafiki yake
aliyekuwa akiitwa Dick Mulungu ambaye alipata daraja la pili katika Shule ya
Sekondari ya Songea Boys, hivyo ikawa rahisi kwake kupata kazi ya ualimu katika
shule hiyo,” alisema mmoja wa waliofanya kazi naye shuleni hapo (jina
tunalihifadhi kwa sasa).
Aliongeza kuwa Mulugo alianza kama mwalimu
wa kawaida, lakini baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Shule (headmaster) wakati
hakuwa hata na cheti cha ualimu. Alichukua nafasi hiyo ya ukuu wa shule baada ya
aliyekuwapo kufariki dunia.
“Unajua wale wahindi (wamiliki) walikuwa ni
wafanyabiashara kwa hiyo hawakufuatilia kiwango cha elimu ndiyo maana
walimpandisha tu madaraja bila kujali kuwango cha elimu,” alisema rafiki yake
huyo na kuongeza:
“Nilimshauri aachane na cheo hicho kwani
kama ungefanyika ukaguzi wa Serikali na kumkuta bila vyeti vya ualimu
angechukuliwa hatua, hivyo alinisikiliza na akaachia nafasi hiyo na kujipa cheo
cha umeneja wa shule.”
Chanzo: mwananchi.co.tz
Chanzo: mwananchi.co.tz
Post a Comment