Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
linatoa pongezi kwa timu ya Azam ya Tanzania Bara kwa kufanikiwa kusonga mbele
katika michuano ya Kombe la Shirikisho iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF).
Ushindi wa jumla ya mabao 8-1 ambao Azam
imeupata dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini si fahari kwa timu hiyo tu, bali
Tanzania kwa ujumla, na unaonyesha jinsi klabu hiyo ilivyojipanga kiushindani
katika michuano hiyo ya Afrika.
Hata hivyo, ni vizuri Bodi ya Wakurugenzi ya
klabu hiyo, benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wakautazama ushindi huo
kama changamoto kwao kuhakikisha wanajipanga vizuri zaidi kwa raundi
inayofuata.
Timu ya Azam inayofundishwa na Mwingereza John
Stewart Hall ilishinda nyumbani mechi ya kwanza mabao 3-1, na jana kuibuka na
ushindi wa mabao 5-0 ugenini jijini Juba.
Kwa kufanikiwa kuing’oa Al Nasir Juba, Azam sasa
watacheza raundi ya kwanza (raundi ya 16 bora) ya michuano dhidi ya Barrack
Y.C.II ya Liberia ambayo katika raundi ya awali iliitoa Johansens ya Sierra
Leone. Barrack ilishinda bao 1-0 nyumbani katika mechi ya kwanza na kulazimisha
suluhu katika mechi ya marudiano jijini Freetown.
Azam itaanzia mechi hiyo ugenini kati ya Machi
15,16 na 17 mwaka huu wakati mechi ya marudiano itachezwa Tanzania kati ya
Aprili 5,6 na 7 mwaka huu.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)
Post a Comment