Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya kuchunguza
kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012 Prof.
Sifuni Mchome (katikati)akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es
salaam kuhusu kuanza kwa zoezi la ukusanyaji wa maoni kutoka wadau mbalimbali.
Wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene (kushoto) na
Bi.Tunu Temu mjumbe wa Sekretarieti ya Tume hiyo.
…………………………………………………………………
Na.
Aron Msigwa -MAELEZO, Dar es salaam.
Tume
ya Taifa iliyoundwa na Mh. Waziri mkuu Mizengo Pinda kuchunguza kushuka kwa
kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne mwaka 2012 imewaomba
watanzania kuipa ushirikiano kwa kutoa maoni yao ili iweze kukamilisha majukumu
iliyopewa kwa muda na ufanisi mkubwa.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa Tume hiyo
Prof.Sifuni Mchome ameeleza kuwa tume hiyo ilianza kazi mara baada ya
kuzinduliwa na Waziri mkuu tarehe 2 mwezi Machi mwaka huu na kufafanua kuwa
jukumu lililopo sasa ni kuanza kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa watanzania ili
kubaini sababu za matokeo mabaya ya mtihani huo.
Amesema kuwa
tume hiyo pamoja na mambo mengine imepewa jukumu la kutoa mapendekezo ya hatua
za kuchukua ili kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha
elimu nchini huku mapendekezo hayo yakizingatia kipindi cha muda mfupi , kati
na kipindi cha muda mrefu.
Prof.
Sifuni ameeleza kuwa tume hiyo inafanya kazi kwa kuzingatia hadidu mbalimbali
za rejea zikiwemo kubainisha sababu za matokeo mabaya ya kidato cha nne 2012,
sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu, nafasi ya Halmashauri katika kusimamia
elimu ya sekondari katika halmashauri zake.
Rejea
nyingine ni pamoja na pamoja na kuanisha sababu nyingine zinazoweza kuwa
zimechangia hali ya matokeo hayo pamoja na kutoa mapendekezo ya hatua za
kuchukua mara moja kwa wanafunzi 240,903 waliofeli mitihani yao kwa kupata
daraja sifuri.
Amefafanua
kuwa tume katika kutekeleza majukumu yake itapitia mitaala na mihutasari ya
Elimu ya Msingi na Sekondari, kutathimini kiwango na mazingira ya ufundishaji na
ufunzaji, kuangalia mfumo wa upimaji na tathmini ya mitihani pia usimamizi na
uendeshaji.
Pia
pamoja na mambo mengine tume itatathmini mchango wa jamii na wazazi/ walezi
katika maendeleo ya wanafunzi, hali ya upatikanaji wa chakula cha mchana,
upungufu wa majengo ya shule,madarasa, maabara
na maktaba.
Vilelevile tume
hiyo itafuatilia mwamko wa wazazi katika kufuatilia mkazo wa eliimu kwa watoto
na suala la mmomonyoko wa maadili unaotokana na ukuaji wa utandawazi hususan
teknolojia ya Habari na Mawasiliano na kutathmini athari ya mfumo wa ufundishaji
wa mikondo miwili iliyopo katika shule za
Zanzibar.
Aidha
mwenyekiti wa Tume hiyo amebainisha kuwa tume itaanza rasmi kukutana na wadau
mbalimbali kwa lengo la kupata maoni kuanzia tarehe 11 mwezi huu kwa kuanza na
mkoa wa Dar es salaam, Zanzbar na maeneo mengine nchini kwa kukutana na viongozi
wa ngazi mbalimbali za Wizara, Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata, Shule, Taasisi
mbalimbali za kijamii na wananchi kwa ujumla na pia kuwasilisha maoni kwenye
tume kupitia Mwenyekiti wa Tume, Tume K4-2012, S.L.P 5909 Dar es salaam au
kupitia simu 0737206038, Barua pepe: maoni@tumek4.go.tz au kwa
kutembelea Tovuti ya tume ya www.tumek4.go.tz.
Post a Comment