Mwendesha mashtaka wa Serikali Basilius Namkambe aliaambia
Mahakama hiyo Mbele ya Jaji Samweli Karua kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa
hilo Mei 15,2011 katika Kijiji cha Mpandapanda kata ya Kiwira Wilayani Rungwe
kinyume na kifungu cha 196(16) kilichofanyiwa marekebisho Mwaka 2002.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Hakimu Mwakalinga ambaye ndiye
mtuhumiwa namba moja katika kesi hiyo akiwa na Daudi Mwasipesya,Obote
Mwanyimbili na Kelvin Maurus Myovela ambao wanatuhumiwa kumuua John Mwankenja
aliyekuwa Diwani wa Kata ya Kiwira(CCM) na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya
ya Rungwe.
Awali baada ya kupandishwa kizimbani watuhumiwa kujibu kesi
inayowakabili yenye namba 31/2012 walimkataa Wakili aliyejulikana kwa jina moja
laMwakabubu aliyekuwa ameteuliwa kwa ajili ya kuwatetea kwa madai kuwa hawana
imani naye kutokana na mwenendo wa kesi alizosimamia.
“Mtukufu Jaji kabla ya kesi yetu haijaanza kusikilizwa tunaomba
kubadilishiwa Wakili kwa sababu huyu Mwakabubu hana uwezo na tumeona kesi ndogo
tu anababaika na kesi yetu ni kubwa tunaona wazi kabisa kuwa hataweza kututetea”
alisema Mwakalinga Mshitakiwa namba moja.
Kufuatia ombi hilo Jaji Karua alikubaliana nao ambapo alimteua
Wakili mwingine ambaye ni Sambwee Shitambala ambaye walimkubali kabla
hajawaongezea wakili mwingine ili asaidiane na Shitambala ambapo alimtaja Wakili
Zakia Selemani.
Akisoma mashtaka yao Mwendesha mashtaka wa Serikali Basilius
Namkambe aliiambia mahakama hiyo kuwa mnamo tarehe 19, Mei 2011 majira ya jioni
marehemu akiwa anatokea Mbeya mjini akirudinyumbani kwake Kiwira Wilayani Rungwe
alifika Nyumbani akiwa na gari lenye namba za usajili T 127ACZ Nissan (Double
cabin).
Namkambe aliongeza kuwa baada ya kufika nyumbani kwake alipiga
honi ya gari kwa ajili ya kuomba kufunguliwa geti la mlango ambapo baada ya
kusikia honi hiyo alitoka Mjomba wake ambaye baada ya kumfungulia aliambiwa
ashushe Kuku aliyokuwa amewabeba nyuma ya gari yake.
Alisema kabla ya mjomba wa Marehemu hajaanza kushusha kuku
kwenye gari alitokea mshitakiwa namba moja akiwa na siraha ambapo alimwamuru
asifanye lolote ndipo akaanza kufyatua risasi akimwelekezea marehemu kisha
kumuuana kutoweka kusiko julikana.
Akijibu tuhuma hizo Wakili wa Utetezi Shitambala na Zakia
walikana washtakiwa hao kuhusika na matukio hayo pamoja na baadhi ya vielelezo
vilivyotolewa na upande wa mashtaka kuthibitisha kuhusika kwa wateja wao.
Walisema mtuhumiwa wa kwanza hakuwepo Wilayani Rungwe siku ya
tukio ambapo walisema atakuwa na mashahidi ambao watathibitisha kwamba
hakuhusika ambao waliwataja kuwa ni pamoja na yeye mwenyewe, Askari Magereza
wawili wa gereza la Tukuyu Wilayani Rungwe waliotajwa kwa jina moja moja la
Hereda na Green.
Wengine ni Padeso Mwakipesile, Aneth Siandene Kalinga na Jumanne
Mwakisole huku washtakiwa namba mbili, tatu na nne ambao hawatakuwa na mashahidi
ambapo watasimama wao wenyewe kujitetea.
Namkambe aliiambai mahakama hiyo kuwa upande wa mashtaka utakuwa
na mashahidi zaidi ya 15 ambao aliwataja kuwa ni pamoja na Sofia Fungameza,
Weston Gilbert,Magdalena Mgawe, Musa Jackson, Issa Mwaipopo, Teresia Ludovick na
Williamu Mtanga.
Wengine ni askari Polisi Mwenye namba D2385 Sajent Michael wa
Tukuyu, Inspekta Isaya Bwile wa Tukuyu, David Paul kutoka makao makuu ya Polisi
Dar Es Salaam, Twaha kutoka kitengo cha Upelelezi makao makuu ya Polisi Dar Es
Salaam, Haruna kutoka Polisi Tukuyu na WP3433 Agnes wa polisi Tukuyu.
Namkambe aliwataja mashahidi wengine katika kesi hiyo kuwa ni
pamoja na aliyekuwa Mkuu wa upelezi (RCO) Mkoa wa Mbeya aliyehamishiwa makao
makuu SSP Anacletus Malindisa, John Mayunga na Dk. D Z Matata kutoka ofisi ya
Mkemia mkuu wa Serikali.
Jaji Karua aliahirisha kesi hiyo hadi hapo itakapopangwa tena
kwa ajili ya kuendelea na kuwasilikiza mashahidi kutoka upande wa mashtaka baada
ya kuambia mahakama kuwa upelelezi umekamilika na mashahidi wote wako
tayari.
Na
Venance Matinya, Mbeya.
Post a Comment