Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, akiwa ndani ya chombo kuelekea Juani, mahali iliko Hospitali ya Wilaya ya Mafia.
Naibu Waziri wa Afya, Mheshimiwa Dk. Seif Rashid, akiongozana na Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mheshimiwa Sauda Mtondoo, wakitembea katika fukwe ya bahari ya Hindi, baada ya kushuka kwenye chombo kuelekea katika mkutano na watumishi wa idara ya Afya.
Baadhi ya watumishi wa serikali, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mheshimiwa Dk. Seif Seleman Rashid, alipokuwa akizungumza nao katika moja ya kumbi za hospitali ya wilaya ya Mafia iliyopo Juani.
********
Na FRANK MBUNDA, Mafia
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mheshimiwa Dk. Seif Seleman Rashid, amewafariji wafanyakazi wa Hospitali ya wilaya ya Mafia, Juani, na kuwataka kuendelea kutoa huduma kwa jamii, wakati serikali ikishughulikia changamoto zinazowakabili.
Dk. Seif alisema kuwa anatambua hali mbaya ya mazingira na kuchelewa kutekelezwa kwa ahadi zinazohusu maslahi ya wafanyakazi hao, lakini hilo lisiwe kigezo cha kukata tamaa na kushindwa kuwasaidia wananchi wenye mahitaji ya huduma yao.
Akizungumza katika ziara yake ya siku moja wilayani humo, Naibu Waziri huyo alisema kwa kuzingatia mazingira ya wilaya hiyo ambayo ni kisiwa, hivyo inahitaji uangalizi maalum (Special Care).
“Ninawaomba kwa dhati ya moyo, mtimize wajibu wenu, mimi ninajua changamoto zinazoikabili sekta hii, kwa hiyo ninaahidi kuwasiliana na wenzetu wa TAMISEMI ili kuona jinsi ya kukabiliana nazo,” alisema Waziri Seif.
Alisema pamoja hali hiyo, lakini watumishi hao wamekuwa waungwana kwa kusimamia viapo vyao vya kazi kwa kutoa huduma kwa jamii bila upendeleo, huku Mafia ikiongoza kwa kukosekana kwa taarifa za unyanyasaji akina mama wajawazito.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Seif, serikali itaanza kufanya upembuzi wa kina kuhusu madai ya watumishi wa sekta hiyo ya afya nchini, lakini kwa hali halisi ya kisiwa cha Mafia, ni lazima upendeleo utaangaliwa ili kuwaweka katika mazingira mazuri.
Alisema akirejea Dar es Salaam, atafanya kikao na Waziri wake Mheshimiwa Dk. Hussein Mwinyi, kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kutafutia ufumbuzi wa haraka mahitaji ya hospitali hiyo ya wilaya.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya hiyo Mheshimiwa Sauda Mtondoo, alimuomba Waziri Seif, kuangalia uwezekano wa kuishawishi wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kutenga fedha kwa ajili ya kuifanyia ukarabati hospitali hiyo.
Pia Mtondoo alisema suala la uchache wa watumishi wa afya ni moja ya changamoto zinazoikabili wilaya hiyo, na kumuomba Waziri Seif, kulichukua na kulifanyia kwa ukaribu zaidi.
Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kusema kwamba maboresho katika sekta hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 hadi mwaka 2012, na kuomba kila mdau kusimama katika nafasi yake ili kukabili changamoto zilizopo.
“Pamoja na suala hilo watumishi, ninaomba kuchukua nafasi hii, kufikisha kwako suala la vifaa tiba, ambalo kwa hakika nalo linatakiwa kufanyiwa kazi kikamilifu, lakini pia wewe uwe balozi wetu,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Mkuu huyo wa wilaya aliwageukia watumishi hao wa afya na kuwataka kufanyia kazi maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri Seif, ili jamii iweze kuendelea kufaidi huduma zao.
Mganga Mkuu wa hospitali hiyo ya wilaya Dk. Credianus Mgimba, alisema pamoja na kuwapo kwa changamoto kadhaa lakini ari ya kazi kwa watumishi hao bado ni nzuri na kuiomba wizara kutowasahau.
“Mheshimiwa Naibu Waziri, sisi ni wadau halisi wa wizara yako, pamoja kwamba kwa sasa tunawajibika TAMISEMI, hivyo msitusahau na kututia unyonge, kwani tunatambua wajibu wetu na tutaendelea kuusimamia,” alisema Dk. Mgimba.
Pia Dk. Mgimba, aliitaka serikali kuangalia uwezekano wa kufanya ukarabati wa majengo ya hospitali hiyo, ili iwe kwenye mazingira yanayovutia na kumridhisha mtumishi anayewajibika hapo.