JESHI la
Polisi mkoani Njombe, limemfukuza kazi askari wake PC Gelvas Joseph, mwenye
namba 9790, kwa kosa la kufanya mauaji ya mwalimu wa Shule ya Sekondari Kitulo,
wilayani Makete.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Mrakibu
Mwandamizi wa Polisi, Focus Malengo, alisema askari huyo alifanya kosa hilo
Februari 27 mwaka huu kwa kumpiga risasi kifuani mwalimu Castory Sote (31), na
kusababisha kifo chake papo hapo.
Alisema askari huyo amefukuzwa kazi baada ya
uchunguzi wa tukio hilo kukamilika na kubaini alikiuka kanuni za utumishi ambapo
hivi sasa anakabiliwa na mashtaka.
Aliongeza kuwa, kosa hilo alilifanya akiwa lindoni
kwenye Benki ya NMB, tawi la Makete, ambapo marehemu alikuwa akichukua fedha
katika mashine za benki hiyo.
Ilidaiwa kuwa, siku ya tukio hilo kulitokea
malumbano kati ya mwalimu huyo na askari ambaye alimtuhumu marehemu kuendesha
pikipiki bila kuvaa kofia ngumu (helmet) kichwani. Hali hiyo ilizua mzozo kati
yao baada ya marehemu kudai kuwa, polisi huyo si askari wa Kikosi cha Usalama
Barabarani.
Post a Comment