Bibi wa miaka 80 Mwajuma Hassani ambaye ni mkazi
wa kata ya Makiba akieleza namna mafuriko yalivyo athiri makazi pamoja na
mashamba
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuigawa misaada hiyo, Makamu mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Frida Kaaya alizitaja kata zilizoathiriwa na mafuriko hayo kuwa ni Makiba, Mbunguni na King’ori ambapo, halmashauri hiyo kupitia kitengo cha maafa ilitenga kiasi cha sh. milioni 30 mapato ya ndani kwa ajili ya kuzinusuru.
Alieleza kuwa, wananchi hao waliathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na mvua kubwa zilizofululiza kunyesha wilayani humo na kusababisha maji kujaa majumbani kwa wakazi hao, ambapo vyakula vyao vilielea juu ya maji, huku mazao waliooteshwa yakisombwa na mafuriko.
Aidha, alisema baada ya kupata taarifa juu ya mafuriko hayo kutoka kwa madiwani wa kata husika, kamati ya maafa ilitembelea na kujionea uharibifu uliojitokea na kulazimika kutafuta kiasi hicho cha fedha ikiwemo kuomba msaada kwa wadau wa halmashauri hiyo na mabenki mbalimbali yaliliyopo mkoani hapa.
Alisema fedha hizo zilitoshea kununua magunia 125 ya Unga wa mahindi pamoja na magunia 30 ya maharage ambapo yaligawanywa kupitia ofisi za watendaji na wenyeviti wa vijiji wakiwemo madiwani wa kata husika.
Wakipokea msaada huo mmoja wa madiwani hao kutoka kata ya King’ori, Akundael Nanyaro, aliipongeza halmashauri hiyo kwa msaada walioutoa kwani itasaidia kunusuru familia zinazokabiliwa na njaa ambazo zinaendelea kuteseka hadi sasa.
Alisema Kata hiyo imeathirika sana kwani baadhi ya nyumba zilibomolewa na mvua hizo, vyoo kufurika na kutoa vinyesi, mifugo kusombwa na maji pamoja na vyakula kuharibika vibaya hali inayohatarisha afya za wakazi hao.
Naye Afisa mtendaji wa kata ya Mbunguni, Godfrey Mollel alivitaja vijiji vilivyokumbwa na athari hiyo kuwa ni Mbunguni, Msitu wa Mbogo, Migungani, Kikuletwa na Shambarai Burka.
Alisema wananchi wa vijiji hivyo hawana chakula, wanaishi kwa kubangaiza na mara nyingi wanashindia mlo mmoja wa mboga za majani aina ya mlenda na maji tu.
Alisisitiza kuwa Kata hizo zipo kwenye hali mbaya na kuitaka Serikali na wadau wengine kujitokeza kuzisaidia zaidi kwani msaada walioupata utasaidia kwa muda mfupi kisha baadaye wataendelea na hali ngumu ya maisha katika maeneo hayo kwa kuwa hawana msaada mwingine kutoka sehemu yoyote.
“Tunaomba pia tusaidiwe mbegu za mahindi, mtama na maharage ili wananchi wapate kupanda upya kwenye mashamba yao ambayo mazao waliyokuwa wameoteza yamesombwa na mafuriko,” alisema Mollel.
Post a Comment