Mkuu wa wilaya ya Singida, mwalimu Queen Mlozi akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya sherehe za muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya Mandewa mjini Singida.
Baadhi ya wakazi wa manispaa ya Singida,waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya sherehe za muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Diwani wa viti maalum (CCM) manispaa ya Singida Yagi Kiaratu akitoa burudani na mzee Juma Ntandu kwenye kilele cha maadhimisho ya sherehe za muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyika katika viwanja vya Mandewa Singida mjini.(Picha zote na Nathaniel Limu).
Na Nathaniel Limu wa Mo blog
Serikali ya wilaya ya Singida, imewaagiza wakazi wake kuimarisha ushirikiano na jeshi la polisi,ili kulinda kikamilifu amani na utulivu ulioasisiwa na muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mkuu wa wilaya hiyo, Queen Mlozi ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, zilizofanyika kiwilaya katika viwanja vya Mandewa Singida mjini.
Amesema ili tuweze kutekeleza ipasavyo shughuli zetu za kiuchumi na kijamii,tunahitaji sana hali ya amani na utulivu.
“Ili tuweze kudumisha amani na utulivu uliopo,kila raia mwema ni lazima awe askari wa mwenzake na tuwe wepesi kutoa taarifa kwa viongozi au vyombo vya usalama kila tunapomtilia mashaka mtu ye yote”amefafanua Mlozi.
Katika hatua nyingine,mkuu huyo wa wilaya,aliwataka wakulima kuacha tabia ya kuuza mazao wakiwa shambani ambayo yananunuliwa kwa bei ndogo mno.
“Niwakumbushe kuwa tuache kabisa tabia ya kuuzia mazao shambani tena kwa bei ya chini.Musimu wa kuvuna baadhi ya mazao ya chakula umeanza,tusisahau kuweka akiba na kutumia vizuri chakula ulichopata,ili tujikinge na njaa.Ni aibu kwa Wanasingida kuomba chakula”,amesema.
Mlozi amesema kuwa wilaya katika msimu huu wa masika, umepata mvua za kutosha hivyo hategemei kupata taarifa za wananchi kuomba chakula mwaka huu wa 2013, labda itokee sababu maalum za msingi.
Aidha, Mlozi amesema mafanikio yaliyopatikana kupitia muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar,hatuna budi kuyasdumisha kwa kufanya kazi halali kwa juhudi na maarifa.
Mkuu wa Wilaya hiyo amesema “Muungano wa Tanzania ni lazima ubaki kuwa ni kiashiria cha muungano miongoni mwetu wananchi.Ni lazima tuoneshe muungano katika shughuli za maendeleo baina ya mtu na mtu, taasisi moja na nyingine, wananchi na serikali yao”.
Post a Comment