Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
DAR ES
SALAAM.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
Profesa Anna Tibaijuka, ametoa siku 30 kwa mmiliki wa jengo la ghorofa 16,
lililopo Mtaa wa Indira Gandhi katikati ya jiji, Ally Raza kulibomoa jengo hilo
baada ya kubainika alilijenga chini ya kiwango.
Kadhalika
Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imeiagiza Halmashauri ya Manispaa ya
Ilala, kufanya uchunguzi wa ubora wa majengo mengine matano yanayomilikiwa na
Raza ambaye pia ni mmiliki wa jengo lingine la ghoroga 16 lililoporomoka wiki
iliyopita jijini Dar es Salaam kama yako katika viwango vinavyokidhi.
Jengo
hilo lililoporomoka lilisababisha vifo vya watu 36, majeruhi 17 na uharibifu wa
mali ikiwamo magari linamilikiwa na Raza.
Jengo
hilo lilikuwa likijengwa na Kampuni ya Lucky Construction Limited ambayo ni mali
ya Diwani wa Kata ya Goba (CCM) Wilaya ya Kinondoni, Ibrahim Kisoki ambaye pia
alijenga jengo jingine jirani na la awali, imetolewa amri ya kufanyika kwa
utafiti kubaini kama limekidhi viwango.
Profesa
Tibaijuka akizungumza mbele ya Kamati hiyo walipofanya ziara katika jengo hilo
jana, alisema uchunguzi wa awali wa kuporomoka kwa jengo hilo umebaini kuwa
jengo lililoko mkabala, pia lilijengwa chini ya viwango.
“Ninaagiza
jengo hilo kuwa libomolewe ndani ya siku 30 kwa gharama za mmiliki na akikaidi
atalipishwa faini ya asilimia mbili ya gharama ya kuendeleza pasipokuwa na
kibali kwa kila siku hadi atakapotekeleza agizo hilo,” alisema Profesa Tibaijuka
na kuongeza;
“Makazi
haya yanatakiwa kujengwa majengo yasiyozidi ghorofa 10, lakini katika hili
ghorofa ambalo linatakiwa kubomolewa kwanza kiutaalamu halikuzingatia vigezo
kutokana na kujengwa kwenye kiwanja chenye mita 150 ambacho ni
kidogo.”
Naye
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli alisema kuna taarifa kwamba mmiliki wa
jengo anamiliki majengo mengine ambayo hivi sasa yanakaliwa na watu pia yamezua
hofu, hivyo yanatakiwa kufanyiwa uchunguzi.
“Kutokana
na majengo yake mawili ambayo tayari yameleta utata kwa kuonekana kujengwa chini
ya viwango, hivyo tunataka majengo mengine anayomiliki, Manispaa ya Ilala
iyafanyie uchunguzi mapema ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea,”
alisema Lembeli.
Naye
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk Terezya Huvisa amewataka
watu wanaotaka kujenga majengo yenye zaidi ya ghorofa sita kufika ofisini kwake
kupata vibali vya ujenzi.
“Mtu yeyote anayetaka
kujenga jengo zaidi ya ghorofa sita anatakiwa kuomba kibali wizarani na wao
kupitia Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) watatoa kibali cha kujengwa au
kutojengwa kutokana na uchunguzi wa sehemu husika,” alisema Dk
Huvisa
Post a Comment