Waziri wa Fedha na Uchumi Mhe Dk. Wiliam Mgimwa akitiliana saini na Balozi wa EU Mhe. Filiberto Sebregondi.
Na Frank Mvungi na Eleuteri Mangi-MAELEZO
SERIKALI ya Tanzania imetiliana
saini mkataba na Jumuiya ya Umoja wa nchi za Ulaya( EU) utakaowezesha
Tanzania kupatiwa shilingi bilioni 20 kusaidia maendeleo katika sekta ya
kilimo cha miwa kwa wakulima wa Visiwa vya Zanzibar.
Mkataba huo umesainiwa leo jijini
Dar es salaam kati ya Waziri wa Fedha na Uchumi Mhe Dk. Wiliam Mgimwa na
Balozi wa EU Mhe. Filiberto Sebregondi, ambapo unategemewa kuisaidia
serikali katika kuondoa umasikini kwa wananchi wake na kuiwezesha nchi
kupiga hatua ya maendeleo kupitia sekta ya kilimo.
Waziri Mgimwa alisema kuwa msaada
huo pia utasaidia kuwajengea wananchi uwezo wa kutekeleza kilimo chenye
tija na kupanua soko la bidhaa zitokanazo na miwa kwani miundo mbinu ya
maeneo ya Uzalishaji pia itaboreshwa katika utekelezaji wa mradi huo.
“Kwa niaba ya Serikali ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania napenda kuishukuru jumuiya ya umoja wa
nchi za Ulaya kwa juhudi kubwa wanazochukua kusaidia maendeleo ya nchi
yetu, asanteni sana,” alisema Waziri Dk.Mgimwa.
Naye balozi wa EU, Mhe. Filberto
Sebrigondi alisema wameridhishwa na mikakati ya serikali katika
kuwaletea wananchi wake maendeleo ndio maana wanaendelea kuunga mkono
juhudi za serikali ili kusaidia wananchi kufikia maendeleo ya kweli
hivyo wameamua kusaidia sekta ya miwa ili iweze kukua na kuchangia
katika maendeleo ya Taifa.
Pia balozi Sebrigondi alisema kuwa
wataendelea kusaidia bajeti ya Serikali ya Tanzania katika miradi
mbalimbali ya maendeleo kwa kuwa Tanzania imeonyesha nia ya dhati katika
kukuza uchumi wake na kuweka mazingira mazuri kwa wananchi wake ili
waongeze tija katika uzalishaji.
Alisema katika kipindi kilichopita
asilimia 87% ya fedha lizizotolewa kwa Serikali ya Tanzania
zimeshatumika katika miradi ya maendeleo, hivyo ameahidi kuwasaidia
wanachi wanaojihusisha na kilimo cha miwa ili kuwajengea uwezo, kufanya
tafiti na kutoa elimu ya utunzaji mazingira katika maeneo
yatakayonufaika na msaada huo.
Umoja wa nchi za Jumuiya ya Ulaya
umekuwa kwa muda mrefu ukisaidia sekta mbalimbali za maendeleo hapa
nchini ikiwa ni moja ya washirika wa maendeleo wa Tanzania ambapo
baadhi ya Sekta zinazonufaika ni sekta ya kilimo cha Kahawa, na Miwa,
sekta ya Barabara, Elimu, nishati ya Umeme ambazo zimesaidia kwa kiasi
kikubwa kukuza uchumi wa Tanzania.



Post a Comment