Katibu Mkuu Maliasili na Utalii Bi. Maimuna Tarishi alianza ziara yake Same kwa kufika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Same Mwalimu Herman Kapufi kujitambulisha.
Mkuu
wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi Donat Mnyagatwa(aliyenyoosha mkono)
akimuonyesha Katibu Mkuu Bi. Maimuna Tarishi (suti nyeusi) eneo lenye
mgogoro wa mpaka katika Hifadhi ya
Mkomazi. Wengine pichani kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Malikale Donatius
Kamambaa; Kaimu Mkurugenzi wa Mipango wa TANAPA Dk. Ezekiel Dembe na
Mkurugenzi wa Utumishi Wizara ya Maliasili na Utalii Said Msambachi.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi Donat Mnyagatwa akitoa Taarifa ya Hifadhi ya Mkomazi kwa Katibu Mkuu Maliasili na Utalii pamoja na ujumbe wake.
Mkuu
wa Hifadhi ya Mkomazi Donat Mnyagatwa (kulia) akimuonyesha Katibu Mkuu
Maliasili na Utalii Bi. Maimuna Tarishi mojawapo ya majengo mapya yaliyojengwa na hifadhi hivi karibuni. Watumishi
wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi wakiwa makini kumsikiliza Katibu Mkuu
Maliasili na Utalii Bi. Maimuna Tarishi alipowatembelea
Katibu Mkuu Maliasili na Utalii Bi. Maimuna Tarishi (wapili kulia) akizungumza
na watumishi wa Hifadhi ya Mkomazi. Wengine pichani kutoka kulia ni
Mkurugenzi wa Malikale Donatius Kamamba, Mkuu wa Hifadhi ya Mkomazi
Donat Mnyagatwa na Mkurugenzi wa Utumishi wa Wizara ya Maliasili na
Utalii Said Msambachi.
Katibu Mkuu Maliasili na Utalii Bi. Maimuna Tarishi katika picha ya pamoja na watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
……………………………………………………
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na
Utalii Bi. Maimuna Tarishi amewataka watumishi wa Hifadhi za Taifa
nchini kuzingatia maadili na weledi katika utendaji kazi wao wa kila
siku ili kudumisha sekta ya uhifadhi nchini. Bi. Tarishi aliyasema hayo
alipokutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi
wilayani Same, Kilimanjaro hivi karibuni.
Bi. Tarishi alisema kuwa sekta ya
uhifadhi nchini inakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo ile ya ujangili
ambayo njia pekee ya kukabiliana nayo ni kuwa na watumishi wenye ari na
moyo wa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na uadilifu.
Alibainisha kuwa ujangili
unaoendelea dhidi ya rasilimali zinazohifadhiwa unapaswa kupigwa vita
kwa kuunganisha nguvu za wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi
zote za uhifadhi kupigana vita moja kwa kuwa wanyama wanaowindwa na
majangili ni walewale na hawana mipaka katika maeneo mbalimbali
yaliyohifadhiwa nchini.
Akizungumzia sekta ya utalii na
hasa kufungua eneo la ukanda wa kusini, Bi. Tarishi alisema kuwa eneo
hili ni eneo mtambuka kwa maana linahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali
na kusema kuwa tayari Serikali imeshaanza kufanyia kazi changamoto ya
miundombinu kwa eneo la ukanda wa kusini ili kuvutia wageni wengi zaidi.
Alitaja kuwa Uwanja wa Ndege wa Mbeya ni mojawapo ya jitihada za
Serikali kuhakikisha kuwa maeneo ya kusini mwa nchi yetu yanafikika kwa
urahisi kwa watalii wanaofika nchini.
Bi. Tarishi ambaye amekuwa katika
ziara ndefu ya kutembelea mashirika na taasisi zilizo chini ya Wizara ya
Maliasili na Utalii aliwapongeza watumishi wa Hifadhi ya Mkomazi kwa
jitihada kubwa walizofanya katika kusimamia uhifadhi ambapo licha ya
hifadhi hiyo kuanzishwa mwaka 2008, tayari mafanikio makubwa yameanza
kuonekana ikiwa ni pamoja na uoto wa asili kurudi kwa haraka na hivyo
kukaribisha wanyama mbalimbali katika hifadhi hiyo.
Post a Comment