WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
Anuani ya Simu “MKUU POLISI” & nbsp; Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi,
Simu : (022) 2110734 Makao Makuu ya Polisi,
Fax Na. (022) 2135556 S.L.P. 9141,
Unapojibu tafadhali taja: DAR ES SALAAM.
8 MAY 2013
TAARIFA YA JESHI LA POLISI KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa kumi na nane wa mwaka kwa Wakuu wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi za Kusini mwa Afrika (SARPCCO) unatarajia kufanyika Mei 15, 2013 jijini Dar es Salaam chini ya mwenyekiti wa umoja huo kwa mwaka 2012/2013 Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania, IGP Said Mwema.
Mkutano huo utatanguliwa na Mkutano wa kamati tendaji za SARPCCO ambao utafunguliwa na IGP Said Mwema Mei 13, 2013 na kufuatiwa na Mkutano wa Wakuu wa Polisi wa nchi hizo utakaofunguliwa Mei 15, 2013 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Dkt Emmanuel Nchimbi.
Katika mkutano huo mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kufanya Operesheni za pamoja na ushirikiano baina ya SARPCCO na Umoja wa Wakuu wa Polisi wa nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO).
Vilevile, mkutano huo utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na Wakuu wa Upelelezi wa SARPCCO pamoja na kamati tendaji za sheria, Mafunzo na kamati tendaji ya Jinsia na watoto katika mkutano wao uliofanyika mwezi Machi jijini Dar es Salaam.
Aidha suala la michezo baina ya Majeshi ya Polisi kwa nchi wanachama nalo linatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo.
SARPCCO iliundwa mwaka 1995 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu. Mpaka hivi sasa umoja huo unaundwa na Nchi kumi na nne ambazo ni Tanzania, Angola, Botswana, Malawi, Lesoto, Mauritius, Congo, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Swaziland na Madagascar.
Imetolewa na:-
Advera Senso-SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Post a Comment