Na Deodatus
Balile, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania inatarajia kukusanya
shilingi bilioni 600 (dola milioni 370) kwa mwezi baada ya mpango mpya wa kodi
kupanua matumizi ya mashine za usajili wa kodi kwa elektroniki (ETR)
zitakazoanza kutumika tarehe 15 Mei.
Ikiwa mpango huo
mpya wa kodi utaonekana kufanikiwa, vituo vya mafuta nchini kote vitatakiwa
kutoa risiti za kodi zilizosajiliwa kwa njia ya elektroniki. Juu, muonekano wa
kituo cha petroli cha TSN katika Barabara ya Bagamoyo jijin Dar es Salaam. [Na
Deodatus Balile/Sabahi]
Kwa sasa, serikali inakusanya shilingi bilioni
400 (dola milioni 250) za kodi kwa mwezi.
Mashine za ETR huorodhesha risiti za mauzo
wakati wa kufunga biashara kila siku na kupeleka data kwa njia ya elektroniki
kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya tathmini sahihi ya kodi.
"Katika mfumo huu mpya, biashara ambazo hupata
idadi yoyote ya fedha kuanzia shilingi milioni 14 (dola 8,600) hadi shilingi
milioni 40 (dola 25,000), kuanzia sasa zitatakiwa kutumia mashine za ETR,"
alisema Naibu Kamishna wa TRA kwa Mapato ya Ndani Generose Bateyunga. Huko
nyuma, biashara hizi ziliweza kukisia tu kodi zao.
Bateyunga aliiambia Sabahi kuwa kiasi cha
walipa kodi 200,000 wamekuwa wakikwepa kulipa kodi au kulipa kiwango cha chini,
na kuongeza kwamba misaada kutoka kwa wafadhili imekuwa ikipungua, kwa hivyo
Tanzania lazima ipanue wigo wake kwa ajili ya kugharamia maendeleo.
Mashine za ETR
zimeunganishwa moja kwa moja kwa intaneti na Mamlaka ya Mapato Tanzania na
zinaweza kutoa hesabu za risiti za mauzo ya kila siku. [Deodatus
Balile/Sabahi]
Mwaka 2010, wakati Tanzania ilipoingiza mashine
za ETR, ukusanyaji kodi uliimarika kwa asilimia 9.6 kwa mwaka wa fedha 2010-2011
na asilimia 23 kwa mwaka 2011-2012. "Tunatekeleza awamu mbili, ambazo
zitawajumuisha hata walipa kodi zaidi," alisema.
Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Walipakodi
TRA Richard Kayombo alisema kuwa mamlaka iliamua kutumia ETR kutokana na ugumu
wa kusimamia mauzo kwa risiti zilizotolewa kwa mkono, kwa vile wafanyabiashara
wasio waaminfu wamekuwa wakitangaza viwango vya chini vya mauzo yao au kutotoa
risiti kabisa.
"Sasa tunaanzisha kampeni kubwa kwa watu wadai
risiti kwa chohote wanachonunua. Hata kama ni pombe, soda au sindano yenye
thamani ya shilingi kumi, chukua risiti," aliiambia Sabahi. "Tunawataka
Watanzania sio tu wadai risiti, bali kuhakikisha kuwa risiti zao ni risiti za
ETR na zinaonesha kiwango halisi walicholipia."
Kayombo alisema kuwa mtu yeyote anayeuza kitu
chochote bila ya kutoa risiti za ETR atajitia hatari ya kupigwa faini ya
shilingi milioni 3, (dola 1,900) hapo hapo au mara mbili ya kiwango hicho kwa
kodi aliyokwepa, ambayo inaweza kuwa zaidi.
Kamishna Mkuu wa TRA Harry Kitilya alisema kuwa
katika awamu hii ya pili, hata vituo vya petroli sasa vitatakiwa kutoa risiti za
ETR.
"Tumeanzisha mradi wa majaribio kwa vituo vya
petroli vya Engen ili kujaribu mashine zetu za ETR zilizounganishwa na pampu,"
aliiambia Sabahi. "Kuanzia sasa, unapoinua mkono wa pampu, mashine inaanza
kuhesabu kiasi gani umetumia. Wakati mkono wa pampu unaporejeshwa sehemu yake,
mashine inatoa risiti yenyewe."
Katika mfumo huu mpya, pampu haziwezi
kumhudumia mteja mwengine kabla ya kutoa risiti ya mteja aliyetangualia,
alisema.
Kitilya alisema kuwa kulingana na mafanikio ya
awamu ya pili, TRA inaweza kuanzisha mfumo wa ETR kwa wafanyabiashara wote nchi
nzima ili kupunguza malalamiko na kuongeza ufanisi.
Potian Michael, mmiliki wa kampuni ya kulehemu
jijini Dar es Salaam, alisifia umauzi wa serikali wa kupanua matumizi ya mashine
za ETR. Katika mfumo wa zamani, alikuwa akilipa zaidi kwa vile TRA ilikuwa
inatathmini zaidi mauzo yake, alisema.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa AP Media na PR
Consult Limited Peter Keasi alisema kuwa kupanua wigo wa kodi ni jambo zuri,
lakini akaelezea wasiwasi wake juu ya uwezo wa serikali wa kubadilisha tabia za
watu.
Watanzania hawajazoea kudai risiti wakati
wanaponunua bidhaa au huduma, alisema, kwa hivyo kampeni ya kubadilisha hilo
inapaswa kuwa kubwa sana, na serikali lazima ihakikishe kuwa mashine za ETR kwa
kweli zinanasa shughuli zote za biashara katika mitaa yenye masoko.
Chanzo: sabahionline.com
Post a Comment