Watu 3,272 kati ya 13,702 wanaoishi na virusi
vinavyosababisha ugonjwa hatari wa UKIMWI waliosajiliwa mkoani Singida, wameacha
matibabu na hawajulikani waliko.
Mkuu wa mkoa wa
Singida. Dk. Parseko Kone (katikati) akitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari
(Picha /Nathaniel Limu)
Hayo yamesemwa na Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt.
Parseko Vicent Kone wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwenye hafla ya
uzinduzi wa mkakati wa ‘Tubajali afya yako rejea kwenye tiba’ iliyofanyika
kwenye viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa mjini Singida.
Amesema kuwa watu hao 3,272 walikuwa wakipatiwa
tiba na matunzo na sasa imepita miaka saba hawaonekani katika vituo vya tiba na
matunzo na hivyo, haijulikani endapo wanaendelea na tiba husika au la.
“Kitendo cha watu 3,272 kutokujulika ni wapi
wanapata tiba,si suala la kulinyamazia kwani lengo la taifa letu ni kwamba kila
mwananchi apate huduma bora za afya,ili aweze kumudu maisha yake na kuisadia
jamii kwa ujumla”amefafanua Dkt. Kone.
Aidha, mkuu huyo wa mkoa, amesema serikali na
wadau mbalimbali wanaendelea kuunganisha nguvu ili kuhakikisha watu wanaoishi na
virusi vya UKIMWI, wanapata huduma bora za tiba na matunzo.
Dkt. Kone alitumia fursa hiyo kubainisha baadhi
ya sababu zinazochangia watu kuacha tiba na matunzo kuwa ni pamoja na kuimarika
kwa afya zao, unyanyapaa, uoga-kuogopa kujulikana kama wanatumia dawa, kukata
tamaa, itikadi za kidini na imani potofu kwamba waganga wa jadi wanaponya
UKIMWI.
Awali Kaimu meneja wa TUNAJALI mkoa wa Singida
Christopher Hamaro, alisema mradi huo unaofadhiliwa na watu wa Marekani kupitia
shirika lao la misaada la USAID, kuwa mradi huo ni endelevu.
Hamaro alisema kuwa mkakati huo,unalenga
kuwarudisha kwenye tiba wale walioanzishiwa ARVs,kuwasaidia kubaki kwenye
matibabu na kuchukua hatua zitakazolenga kuwawezesha wale ambao bado hawatumii
ARV lakini wanastahili kuzitumia,kuanzishiwa dawa hizo.
Post a Comment