Na: Albert Sanga, Iringa
Wiki
iliyopita niliandika makala iliyokuwa na kichwa, “Imani yako inasadifu
fedha zako”. Kama ilivyo ada nimepokea mirejesho mingi kwa baruapepe,
simu za miito na jumbefupi. Wasomaji wamekuwa na mitazamo tofauti
tofauti wengine wakiipongeza makala ile na wengine wakionesha
dukuduku.Pia wapo wachache wamepinga kabisa uthubutu wangu wa kuchambua
fedha katika sura ambayo wanadai nahamasisha watu kutafuta fedha. Hawa
ni wale ambao wanaamini “fedha si nzuri kwa sababu inaharibu tabia za
watu” Nilivutiwa sana na mchango wa msomaji mmoja kutoka Arusha
aliyeniandikia baruapepe ifuatayo, “Bw. Sanga nakupongeza sana kwa
makala zako. Unaandika ujasiriamali na mambo ya kujitambua in unique
style kiasi kwamba kila ninaposoma makala zako napata ladha na impact
kubwa mno. Kwenye makala yako ya...
leo umeeleza vizuri mno kuhusu imani za fedha”
“Loo!
Makala hii imenisaidia na kuniokoa mno kwa sababu nimekuwa na kawaida ya
kushiriki gossiping kuhusu wenye fedha. Mfano hili la kuamini kuwa kuna
makabila yanafanikiwa kwa sababu ya wizi ama ushirikina nimekuwa
ninaamini pasipo kujua kuwa ninaathiriwa na imani hizo”.
“Hata
hivyo Bw. Sanga ninaomba unisaidie nawezaje kuzalisha fedha za
kunitosha? Kwa sababu mimi ni mwajiriwa lakini kadiri siku zinavyoenda
ninaona majukumu yanaongezeka na mshahara naona hautatui mahitaji yangu
vizuri, maisha ni magumu, nikitafiti naona biashara karibia zote
zimeshafanyika, Je, nitafanya kitu gani ama namna gani ili niweze
kuzalisha fedha? Narudia tena kukupongeza na ninaamini utanisaidia
katika hili” Mwisho wa kunukuu.
Katika
makala haya leo ninajibu swali la msomaji huyu aliyeniuliza, “Nawezaje
kuzalisha fedha za kunitosha?” Hata hivyo kabla sijaeleza namna gani mtu
unaweza kuzalisha fedha za kukutosha, ninapenda kueleza kidogo kuhusu
dukuduku walilokuwa nalo baadhi ya wasomaji kuwa fedha siyo nzuri kwa
sababu zinaharibu tabia za watu.
Kimsingi
fedha imebeba chembechembe nyingi za kisaikolojia zenye uwezo mkubwa wa
kuamsha tabia za mtu hata zile ambazo hazijapata kuonekana. Mtu mchoyo
akipata fedha uchoyo wake unaongezeka na unakuwa dhahiri. Mtu mwema na
mtoaji akipata fedha wema wake huongezeka na ataonekana akitoa zaidi na
zaidi.
Kwa jinsi
hii tunaona kuwa kimsingi fedha haibadilishi wala kutengeneza tabia ya
mtu isipokuwa fedha hudhihirisha tabia na hulka aliyonayo mtu ambayo
alishakuwa nayo hata kabla hajaipata fedha. Fedha naweza kuifananisha na
mfumo wa mashine za sauti “Amplifier”.
Kwenye
“Amplifier” ukitoa sauti yako kama ni sauti mbaya ubaya huo utakuzwa na
kama sauti yako ni nzuri basi uzuri wa sauti yako utakuzwa vile vile.
Kwa kuwa fedha zina mfumo wa kukuza tabia, ni vema sana mtu akatumia
muda na rasirimali maarifa kujenga tabia na hulka zake ili fedha
inapokuja isilete mushkeli.
Na
ninapotaja habari ya mtu kuwa na fedha isidhaniwe kuwa ninagusia fedha
nyingi sana, la hasha! Watu tunatofautiana sana linapokuja suala la
mitazamo na hulka zetu katika fedha. Wapo watu ambao akiwa na elfu kumi
tu mfukoni lazima ujue kwa maana ataleta vurugu na maujiko kibao.
Mtu
mwingine akiwa na hiyo shilingi elfu kumi mfukoni haoni kama ana fedha,
isipokuwa anaweza hata kukueleza kuwa “sina fedha kabisa”. Kwa mwingine
milioni moja sio fedha wakati kwa mwingine milioni moja ni utajiri!
Kinachofanya
mtu mmoja aone kuwa elfu kumi ni fedha na mwingine aone kama si fedha
inatokana na mtazamo wanaokuwa nao watu hawa katika fedha. Mtazamo huu
hauanzi pale mtu anapoishika hiyo elfu kumi, isipokuwa ni kuwa mtazamo
wao ulishajengeka mapema kabla hata ya kushika hiyo fedha.
Baada ya
kusema hayo sasa nigeukie upande mwingine kulijibu swali la msomaji
Yule, “Je, nawezaje kuzalisha fedha?”. Kwa wale wenye kumbukumbu bila
shaka wangali wanaikumbuka makala niliyopata kuiandika wiki chache
zilizopita iliyokuwa na kichwa, “Tumeamua kuichuuza thamani ya fedha
yetu”.
Katika
makala hiyo nilieleza kwa kina dhana na maana ya fedha, lakini pia
nilisema fedha sio mafanikio zikisimama peke yake; isipokuwa fedha ni
matokeo ya mtu kufanikiwa. Fedha inatakiwa kumjia mtu baada ya kuzalisha
thamani fulani katika uchumi. Hapa tunaangalia maeneo kadhaa
zinakopatikana fedha.
Kunapotokea
mdororo wa uchumi, mara nyingi mitaani huwa tunasema fedha zimepotea,!
fedha hazionekani,! Kitu cha kujiuliza ni “Je, fedha zinapopotea ama
kutoonekana zinakuwa zimepotelea wapi?” Ukweli ni kuwa fedha zote
zilizopo duniani zinazunguka miongoni mwa watu. Idadi ya fedha huwa
haipungui, ila kinachopungua ama kuongezeka ni thamani ya fedha.
Ukiwa na
fedha leo na kesho ukawa huna basi ujue fedha zipo kwa watu. Kwa maana
hii ukitaka kupata fedha ni lazima uzitafute kutoka kwa watu. Fedha
zinapatikana kutoka kwa watu. Je, unazipataje fedha kutoka kwa watu?
Watu
katika maisha ya kila siku wanakabiliwa na changamoto na matatizo
mbalimbali. Unapochukua wasaa wa kutatua changamoto na matatizo yao ni
lazima utapokea ujira wa utatuzi wako. Hii ina maana kuwa wakati wote
ikiwa unahitaji fedha ni lazima uwe ni mtu unaetazama matatizo na
changamoto kama fursa za kukusaidia kupata fedha.
Tunaposikia
kuwa Tanzania inakabiliwa na tatizo kubwa la ajira; kuna makundi mawili
ya watu yanayolitazama hili kwa mitazamo tofauti. Mosi wapo wale
wanaosimama upande wa kulalamika na wakitazamia kuhurumiwa. Ni vema
wasomaji mkafahamu siri hii: kihisia, fedha ni kama ina masikio, haitaki
malalamiko haitaki manung’uniko!
Ukizoea
kulalamika na kunung’unika ovyo unaifukuza fedha! Lakini ukichunguza
upande wa hawa walalamishi na wanung’unikaji sana; utagundua kuwa wengi
wao huamini kuwa kushindwa kwao ikiwemo kiuchumi(kifedha) ni matokeo ya
uzembe ama kutokuwajibika kwa wengine.
Kundi la
pili ni wale wanaofikiri namna ya kuikabili na kuitatua changamoto hii.
Ndani ya kundi hili la pili ndimo wanakopatikana wale wanaoamua
kujiajiri lakini ninaowakusudia zaidi hapa ni wale wanaowasaidia wengine
kujiajiri. Hawa ni kundi la watu wanaoamua kufanikiwa katikati ya
matatizo na changamoto.
Ndio
maana ukichunguza kwa umakini utabaini kuwa, watu wanaofanikiwa katika
jamii zetu katika maeneo mbalimbali (ikiwemo kifedha) huwa wako “bize”
na mambo yao, hawana muda wa kulalamika wala kunung’unika ovyo.
Wanaofanikiwa mara zote huwa hawawanyooshei vidole watu wengine kutokana
na kushindwa kwao. Wanaofanikiwa huamini kuwa wanawajibika kwa sehemu
kubwa katika mafanikio yao.
Kwa
kuwasaidia wengine kuweza kujiajiri kundi hili hufanikiwa kujipatia
fedha. Unapotatua changamoto ama tatizo lolote kiubunifu ni lazima
unufaike. Tunatakiwa tufahamu kuwa matajiri wote duniani wameupata
utajiri wao kwa kutatua changamoto na matatizo waliyoyabaini miongoni
mwa watu. Fedha zinapatikana kwenye matatizo na changamoto
Tunapoangalia
kuwa fedha zinapatikana kwa kutatua changamoto na matatizo tunajiuliza,
Je, unawezaje kutatua hayo matatizo na changamoto? Jibu lipo hivi: Ili
kutatua tatizo ama changamoto ni lazima ubuni bidhaa na huduma
zinazojibu matatizo na changamoto hizo. Watu walipoonekana wanatembea
peku na kuhatarisha afya zako, alitokea mtu akabuni viatu.
Mpaka leo
tunawalipa wanaotengeneza viatu. Baada ya kuona watu wanahitaji
kusafiri kwa haraka na kwa ufanisi, walitokea waliogundua ndege na hadi
leo tunawalipa watu mbalimbali wanaofanikisha usafiri huo kila
tunapotaka kusafiri. Kila bidhaa unayonunua ama huduma unayolipia
unatakiwa kutambua kuwa ni matokeo ya ubunifu wa wajasiriamali
uliochagizwa na changamoto na matatizo waliyaona miongoni mwa watu.
Wapo
wajasiriamali mbalimbali ambao wamechangamkia fursa zilizotokana na
ukosefu wa ajira na sasa wameanzisha makampuni yanayotoa huduma za
kiushauri na kimafunzo kuwawezesha watu kujiajiri. Hivyo tunaona kuwa
eneo jingine ambako fedha zinakaa ni katika bidhaa na huduma
Njia
rahisi ya kubuni bidhaa na huduma zitakazowavutia wengine kukuletea
fedha ni kutumia karama na vipaji vyako. Kama wewe ni mwimbaji, ukiimba
nyimbo nzuri moja kwa moja utauza nakala na utatumbuiza katika
matamasha. Kama wewe ni daktari mwenye uwezo na kipaji kikubwa cha
kutibu kwa ustadi, ni lazima watu watakuja kupata huduma na kukuletea
fedha. Ndani ya karama na vipaji ndiko zinakopatikana fedha.
Kitu
ambacho tunatakiwa kuepukana nacho ni mawazo ya kupata fedha za
mkato-mkato. Shida ya fedha za mkato-mkato kama ufisadi, wizi, utapeli,
udokozi na uhujumu; sio ile hatari ya kukamatwa na kufungwa jela;
isipokuwa zipo hatari kubwa zaidi ya hapo ambazo ndizo ambazo mimi daima
huzitambulisha.
Ukifanya
ufisadi kazini na ukajipatia fedha kasha ukajenga majumba na kuanzisha
miradi lukuki, hata usipokamatwa usidhani upo salama! Kuna kitu kinaitwa
hukumu ya moyoni “Spiritual Condemnation” ambacho kinaweza kukutesa
sana. “Spiritual Condemnation” ni hatia anayokuwa nayo mtu kwa ndani
kutokana na njia alizotumia kupata fedha zake.
Hili la
madhara ya kutafuta fedha na mafanikio kwa njia zisizohalali linahitaji
makala ya peke yake. Hata hivyo kitu cha kufahamu na kuamini ni kuwa
inawezekana kupata fedha na utajiri kwa njia halali; huna sababu kupita
njia za mikato zitakazokutesa unapofanikiwa. Nihitimishe kwa kusema
kuwa inawezekana na tena ni rahisi kuzaisha fedha ikiwa tutajizoesha
kuyafuatilia na kuzingatia maeneo niliyoyataja ambako fedha
zinapatikana!
Ni haki ya kila mtanzania kuwa na fedha za kutosha
0719 127 901
stepwiseexpert@gmail.com
Post a Comment