Wajane na
wasimamizi wa mirathi zaidi ya 40 wa waliokuwa wafanyakazi wa Mamlaka ya
Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) kutoka Mkoa wa Mbeya, jana
waliandamana katika makao makuu ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii
(NSSF) kudai malipo ya mirathi. Wajane
hao walionekana wakiwa wamefurika katika ofisi za makao makuu ya NSSF
zilizopo jengo la Benjamini Mkapa Tower eneo la Posta, jijini Dar es
Salaam.
Kuwasili
kwa wajane hao kulileta taharuki kwa wafanyakazi wa NSSF makao makuu
kutokana na idadi yao kuwa kubwa hasa ikizingatiwa hakukuwa na taarifa
za ujio wao.
Wakizungumza na NIPASHE nje ya ofisi za NSSF zilizopo ghorofa ya 10
katika jengo hilo, walisema wamewasili Dar es Salaam saa 10:20 alfajiri
kwa treni ya Tazara kutoka Mbeya baada ya kuelezwa kuwa malipo yao
yameiva NSSF makao makuu.
Mkuu wa msafara huo, John Kalinga, alisema hatua ya kwenda Dar es Salaam
kufuata malipo ya mirathi, imetokana baada ya kuelezwa na viongozi wao
pamoja na wafanyakazi wa NSSF Mbeya kuwa malipo hayo yatalipwa huko.
Alisema katika hali ya kushangaza baada ya kuwasili katika ofisi hizo
walielezwa kuwa wamedanganywa kwa kuambiwa kuwa malipo yao yatalipwa Dar
es Salaam.
Kutokana na hali hiyo, Meneja Malipo wa NSSF, ambaye alikataa kutaja
jina lake aliwaeleza wajane na wasimamizi hao wa mirathi kuwa wanatakiwa
kurudi kwa mwajiri wao akawaandikie malipo, ambayo hawakulipwa kwa kila
mmoja na kuwasilisha NSSF.
Ofisa Uhusiano wa NSSF, Eunice Chiume (Chiume), alipotafutwa kwa simu
yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa, badala yake alituma ujumbe kwamba,
muda huo hawezi kuongea na kumtaka mwandishi kutuma ujumbe mfupi wa simu
na alipotumiwa swali hakujibu tena.
Meneja mafao wa NSSF, Oigo James, akizungumza na NIPASHE jana alisema
baada ya wajane na wasimamizi hao kuwasili wamebaini waliowasili ni
wale, ambao ndugu zao walifariki wakiwa kazini na siyo wastaafu.
James alisema wafanyakazi wa Tazara, ambao walifariki wakiwa kazini wote
walishalipwa mafao yao muda mrefu kupitia ofisi ya NSSF Mbeya na hivyo
hakutakuwa na malipo ya ziada.
Hata hivyo, alisema amewashauri wakaonane na mwajiri wao ili kama kuna
malipo, ambayo mwajiri hakuyaweka katika malipo yaliyofanyika awali
awaandikie katika barua ili NSSF iangalie utaratibu kama ni ya kweli na
yanastahili kulipwa.
habari na THOBIAS MWANAKATWE
SOURCE: NIPASHE
Post a Comment