Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abas Kandoro,
Na Anna Nkinda – Maelezo, Mbeya
Watanzania wametakiwa kupiga
magoti na kuomba kila mtu kwa imani yake ili mwenyezi Mungu aweze
kuwalaani watu ambao wanatishia kuvuruga amani ya nchi na kusababisha
chuki katika jamii.
Wito huo umetolewa leo na
Chifu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Rocket Mwashinga wakati akiongea na wakazi
wa Ushirika wilayani Rungwe kwenye mazishi ya George Mwaikela
aliyefariki Dunia juzi jijini Dar es Salaam kwa ajali ya gari.
Chifu Mwashinga alisema kuwa
hali iliyopo nchini hivi sasa si nzuri kwani kuna baadhi ya makundi ya
watu wanataka kuwalambisha watanzania sumu mbaya ya chuki ya udini na
kuwaomba wasiilambe sumu hiyo bali kila mmoja kwa imani yake apige
magoti na kumuomba Mwenyezi Mungu ili amani iliyopo iendelee kuwepo.
“Tunashindwa kulala usingizi
kutokana na hofu na katika mkusanyiko kama huu tunakosa raha kabisa kwa
kuhofia kuwa jambo baya lolote linaweza kutokea”, alisema Chifu
Mwashinga.
Alisema kuwa marehemu George
alikuwa ni kijana mdogo wa kwanza na wa ajabu aliyeweza kuwafuata
mashifu na kuwapa ushauri mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufuata mila
nzuri na kuachana na mila ambazo zimepitwa na wakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa
wa Mbeya Mh. Abas Kandoro alisema kuwa binadamu anaweza kupata madhara
kwa kutokumtii Mwenyezi Mungu na katika kitu kibaya ambacho kinaanza
kutokea katika jamii ya watanzania ni pamoja na kubaguana katika misingi
ya dini hali ambayo itasababisha watu kuuana.
Mh. Kandoro alisema,
“Tumekusanyika hapa kuja kumzika ndugu yetu si kwa itikadi ya dini bali
ni binadamu mwenzetu, tulikuwa tunaishi naye kwa amani na upendo na sisi
sote mbele ya Mwenyezi Mungu ni kitu kimoja na matendo yetu katika
dunia ndiyo yatakayotufanya tuuone ufalme wa Mungu.
Sisi kama viongozi wenu wa
Mkoa huu tunawaomba mdumishe amani na utulivu tulionao ili tuweze
kufanya mambo makubwa kama wanayofanya watu wengine”.
Naye Baba Paroko wa Parokia
ya Roho Mtakatifu Ruanda Padre Peter Malya aliwataka watanzania kuishi
maisha yanayoendana na ubinadamu na ya kumpendeza Mwenyezi Mungu na
kuachana na matendo ya kinyama.
Padre Malya alisema kuwa hivi
sasa kuna baadhi ya watu wanauza mkaa, juu ya magunia wanapanga mkaa
mkubwa na mzuri lakini chini wanaweka chenga na wengine wanauza nyanya,
juu ya ndoo wanaweka kubwa na nzuri lakini chini wanaweka ndogo na
wengine wamefikia hatua ya kuhifadhi samaki kwa kutumia dawa za
kuhifadhia maiti.
“Ninawaomba muishi kwa upendo
na kuwasaidia watu wasiojiweza wakiwemo yatima, wajane, wagonjwa na
vikogwe na kwa kufanya hivyo mtakuwa mnajiongezea baraka kwa Mwenyezi
Mungu na kuacha kumbukumbu pale ambapo mtakuwa mmeaga Dunia na
kutangulia mbele za haki”, alisema Padre Malya.
Viongozi mbalimbali wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali walihudhulia mazishi hayo akiwemo Mke wa
Rais Mh. Mama Salma Kikwete na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika Mh. Adam Malima
Post a Comment