Huku dola ikiahidi kuwakamata watuhumiwa, mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya (43) jana alizikwa huko Kairo, Mirerani, Simanjiro katika mazishi yaliyohudhuriwa na watu wengi wakiwamo vigogo wa Serikali.
Miongoni mwa vigogo waliohudhuria mazishi
hayo ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Maselle ambaye aliwasilisha
salamu za rambirambi za Rais Jakaya Kikwete. Wengine waliokuwapo ni Mkuu wa Mkoa
wa Arusha, Magesa Mulongo, Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka na Naibu
Kamishna wa Polisi, Lazaro Mambosasa, ambaye alimwakilisha Mkuu wa jeshi hilo,
IGP Said Mwema.
Katika mazishi hayo yaliyokuwa na watu wengi
kiasi cha Kamati ya Mazishi kulazimika kusitisha utoaji wa heshima za mwisho,
Mulongo alisema wauaji wa Msuya watasakwa na kufikishwa mahakamani wiki
ijayo.
“Waliomuua Msuya wataumbuka mchana kweupe
wiki ijayo watakapofikishwa mahakamani. Nawahakikishia kuwa vyombo vya dola viko
kazini na ukweli kuhusu waliohusika na tukio hili la kinyama utajulikana
hadharani wiki ijayo wahusika watakapofikishwa mahakamani,” alisema Mulongo
katika ibada ya mazishi iliyoongozwa na Askofu wa KKKT la Dayosisi ya Meru, Paul
Akyoo.
Mambosasa alisema IGP Mwema amewaagiza
polisi katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro kuwasaka na kuwafikisha
mahakamani wahusika wote bila kujali majina, ukwasi wala vyeo
vyao.
Maselle alisema Rais Kikwete ameshtushwa na
kusikitishwa na mauaji ya Msuya aliyekuwa mfanyabiashara maarufu katika mikoa ya
Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro.
Aliwataka wote walioguswa na kifo hicho kuwa
na subira na uvumilivu kwa kuondokewa na mpendwa wao huku akiahidi kuwa vyombo
vya dola vitafanya uchunguzi na upelelezi wa kina kuhakikisha wahusika wanatiwa
mbaroni na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Askofu Akyoo alikemea utajiri wa dhuluma na
kafara.
Katika mahubiri yake yaliyochukua dakika 30,
alisema utajiri wa aina hiyo hauna baraka wala amani kwa wahusika kutokana na
dhamira zao kuwasuta kila wanapokumbuka uhalifu walioutenda.
Mwili wa Msuya ulifikishwa Kairo saa nne
asubuhi kutoka Arusha kwa msafara wa magari ya kifahari zaidi ya 150 pamoja na
mabasi madogo 10 yaliyobeba waombolezaji.
Msuya aliyeuawa kwa kupigwa risasi na watu
wasiojulikana Agosti 7, mwaka huu, aliteremshwa kaburini saa 10:20
jioni.
Mwananchi
Post a Comment