Mwenyekiti wa Chama cha demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) amesema amenusurika kuuawa katika matukio matatu yanayotokana na
harakati zake za kisiasa.
Akihutubia umati mkubwa wa wananchi katika mji
wa Meatu mkoani Simiu jana, Mbowe alisema hata kama atauawa hatasikitika na
kwamba Watanzania wasimlilie.
Mbele ya umati huo akiwemo mbunge wa Maswa,
John Shibuda, Mbowe alisema kuna watu ndani na nje ya CHADEMA ambao wamekuwa
wakifanya kila mbinu kuwaangamiza viongozi na makada wa chama
hicho.
Mbowe alisema viongozi wa CHADEMA akiwemo yeye mwenyewe
wamekumbana na misukosuko mingi, ikiwemo yenye kuhatarisha maisha yao kutoka kwa
wanasiasa wasioipenda nchi, lakini kwa neema ya Mungu
wamenusurika.
“Leo hii hata kama nikiuawa, naomba Watanzania
msinililie. Mbele ya jeneza langu, nizikeni huku mkisema Bwana Alitoa na Bwana
Ametwaaa, Jina Lake Lihimidiwe.
“Leo CHADEMA sio ya Slaa wala ya Mbowe
bali ya Watanzania iliyojengwa kwa misukosuko mingi na mkono wa
Mungu.
“Mmeshuhudia namna viongozi wake walivyonusurika kuuawa na
kufungwa, na watu kufunguliwa na kesi mbalimbali.
“Kwa hiyo yeyote awe
kiongozi wa CHADEMA au watawala anayetamani kuibomoa chadema hataweza kamwe,”
alisema.
Kiongozi huyo alisema wale wote wanaofanya hivyo, wajue kuwa
wanapambana na mkono wa Mungu na wamelenga kuwaumiza Watanzania.
“CHADEMA
ina baraka za Mungu na ndio maana imeshinda na kupita katika majaribu mengi ya
watawala ambao wameshindwa kuifuta au kuibomoa,” alisema.
Mbowe na
viongozi wengine wa CHADEMA wako katika ziara ya mikutano ya mabaraza ya wazi
kujadili rasimu ya Katiba mpya ambayo itaendeshwa nchi nzima kwa nia ya
kukusanya maoni ya Watanzania.
on Wednesday, August 14, 2013
Post a Comment