Mshambuliaji
aliyetokea kukonga mioyo ya mashabiki wa Simba kwa kufumania nyavu,
Betram Mwombeki amekwaa kisiki katika usajili wake kuichezea timu hiyo
baada ya kuwekewa pingamizi na klabu yake aliyoichezea msimu uliopita,
Pamba ya Mwanza.
Awali
iliripotiwa kuwa Mwombeki amesajiliwa na timu hiyo akitokea nchini
Marekani, hata hivyo Pamba wamepinga taarifa hizo na kusema kuwa
mchezaji huyo aliichezea timu yao Ligi Daraja la Kwanza na kufunga mabao
mawili msimu uliopita.
Mwenyekiti
wa Pamba, Kazimoto Miraj Muzo aliiambia Mwananchi kuwa Mwombeki alikuwa
Marekani miaka ya nyuma na mwaka jana alijiunga na Pamba wakati wa
dirisha dogo la usajili na kucheza mechi kadhaa tofauti na taarifa kuwa
ametokea Marekani.
Muzo
alisema kuwa hakuweza kucheza mechi nyingi kutokana na kukabiliwa na
maumivu ya goti. “Si kweli kuwa ametokea Marekani, tupo hapa na
aliichezea timu yetu. Tuliwaambia Simba, wakabisha na sasa tutakutana
mbele ya sheria,” alisema Muzo.
Alifafanua
kuwa walizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are
kuhusiana na usajili wa mchezaji huyo, lakini hakuonyesha kujali taarifa
hiyo.
“Tumewasilisha
vielelezo vyetu TFF, tunasubiri matokeo ya kikao cha Kamati ya Alex
Mgongolwa kutoa uamuzi wake, tumedhamiria kupigania haki yetu mpaka
mwisho” alisema.
Alisema
kuwa kiasi gani cha fedha watakachoidai Simba iwalipe ni siri, kwani
daima wao huwa hawapendi kuweka hadharani masuala ya fedha, hasa za
kumuuza mchezaji.
Itang’are
alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo alithibitisha kuongea na Pamba na
kuahidi kulifanyia kazi. “Pamba ni ndugu zetu, miaka ya nyuma walitupa
wachezaji wengi kama Hussein Marsha, John Makelele, George Masatu, Juma
Amir na wengine, na kwa hili sidhani kama tutashindwana,” alisema
Itang’are.
Wakati
Simba inakabliwa na kikwazo kuhusiana na Mwombeki, Yanga inaelekea
kupeta kwa mchezaji, Mrisho Ngassa kutokana na ukweli kuwa Simba
hajawasilisha taarifa nyingine zaidi ya mkataba tu.
CHANZO CHA HABARI HII NI GAZETI LA MWANANCHI
Post a Comment