THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE
OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hakuna
shughuli za biashara haramu ya binadamu inayofanywa katika Tanzania bali
barabara za Tanzania na ardhi yake inatumiwa kupitisha biashara hiyo.
Hata hivyo, Rais Kikwete
amesema kuwa Serikali yake itaendelea kushirikiana na nchi jirani kuhusu
chimbuko la biashara hiyo na katika kuchukua hatua za kukomesha vitendo hivyo
haramu.
Rais Kikwete ametoa
msimamo huo wa Tanzania leo, Jumatano, Septemba 25, 2013, wakati alipokutana na
kufanya mazungumzo na ujumbe wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani la Millennium Challenge Corporation (MCC)
ukiongozwa na Mtendaji Mkuu wake, Bwana Daniel W. Yohannes.
Ujumbe huo ulikutana na
Rais Kikwete katika Hoteli ya JW Marriott, mjini New York, ambako amefikia kwa
ziara yake ya kikazi nchini Marekani na Bwana Yohannes na wenzake walikuwa
wanamwelezea Rais Kikwete maendeleo ya ombi la Tanzania la awamu ya pili ya
misaada ya maendeleo baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza.
Katika mazungumzo hayo,
Bwana Yohannes ametaka kujua hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali ya Rais
Kikwete kukabiliana na baadhi ya mambo yanayojitokeza kuwa changamoto katika
utekelezaji wa miradi ya MCC kupitia
Shirika la Tanzania la Millennium
Challenge Account Tanzania – MCA (T).
Baadhi ya changamoto
ambazo Bwana Yohannes amezitaja ni pamoja na nini kinafanyika kuhusu TANESCO,
kuhusu juhudi za kupambana na rushwa na jinsi gani ya kukabiliana na biashara
haramu ya binadamu.
Rais Kikwete ametoa
majibu ya changamoto zote tatu na kumweleza Bwana Yohannes kuwa biashara haramu
ya binadamu haifanyiki wala kuanzia katika Tanzania na kuwa inaanzia Ethiopia,
inapitia Kenya, Tanzania, Malawi na kwenda hadi Afrika Kusini.
“Wanakusanya watu katika Ethiopia na kuna mtu
anapewa fedha na watu hao wanaokusanywa. Wanakuja Kenya na kuna mtu wa
kuwapokea na kuwahudumia, wanakuja Arusha na hatimaye wanaingia Malawi na
Afrika Kusini. Katika Tanzania wanapita tu na kuna wakati tulipata kukamata
Waethiopia kiasi cha 19,000 na tukawarudisha kwao kwa gharama yetu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kutoka Ethiopia watu hawa wamekuwa kama mto
usiokauka maji. Hivyo, sisi katika Tanzania tunafanywa kama njia ya kupitia tu.
Ni kweli wako mawakala lakini kwa hakika biashara hii haifanyiki katika
Tanzania. Inafanyika kwingine na nchi yetu inafanywa kama njia tu. Kuna wakati
nilipata kuzungumza na viongozi wa Ethiopia na Kenya kuhusu suala hilo lakini
bado tutaendelea kulifuatilia.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
25 Septemba, 2013
Post a Comment