JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UCHUKUZI
Waziri wa Uchukuzi wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe (MB) na Waziri wa Uchukuzi wa
Singapore, Mhe. Lui Tuck Yew, wamesaini Mkataba wa Huduma za Usafiri wa Anga
kati ya Tanzania na Singapore. Mkataba huo umesainiwa kwenye ofisi za Makao
Makuu ya Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (International Civil
Organization – ICAO), jijini Montreal, Canada. Mhe. Mwakyembe yupo Canada
kuhudhuria Mkutano Mkuu wa ICAO ulioanza tarehe 24 Septemba, 2013.
Kusainiwa kwa Mkataba wa Huduma za Usafiri wa
Anga ni utekelezaji agizo la Marais wa nchi hizi mbili lililotolewa mwezi Juni,
2013 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete
alipotembelea Singapore. Wakati wa ziara ya Mhe. Rais nchini Singapore, Marais
wa nchi hizi mbili waliziagiza Wizara za Uchukuzi kukamilisha Mkataba huo
mapema.
Kusainiwa kwa Mkataba huo kunawezesha mashirika
ya ndege ya nchi hizi mbili kuanzisha huduma za usafiri wa anga na hivyo kutoa
fursa kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kusafiri moja kwa moja kati ya
nchi hizi mbili. Hatua hii itatoa unafuu kwa wasafiri kwa kupunguza muda na
gharama za safari. Mkataba huo pia unatarajiwa kufungua fursa za kiuchumi na
kijamii kati ya nchi hizi ikiwemo utalii na biashara.
IMETOLEWA
NA WIZARA YA UCHUKUZI
24
SEPTEMBA, 2013.
Post a Comment