*KAMATI YA RUFANI YA MAADILI YAFANYA MAPITIO
Kamati
ya Rufani ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
imekutana jana (Oktoba 13 mwaka huu) kusikiliza maombi ya mapitio
(revision) na mwongozo ya uamuzi wa Kamati ya Maadili.
Sekretarieti
ya TFF iliwasilisha maombi ya mapitio kwa Kamati hiyo ya juu kabisa ya
masuala ya maadili kutokana na ugumu wa utekelezaji wa uamuzi wa Kamati
ya Maadili juu ya mashauri nane yaliyowasilishwa mbele yake.
Kamati
ya Rufani ya Maadili itaendelea na kikao chake kesho (Oktoba 15 mwaka
huu), na baadaye itakutana na waandishi wa habari (saa 10 jioni) kwa
ajili ya kutangaza uamuzi wake juu ya mwongozo ulioombwa na Sekretarieti
ya TFF.
*KESSY KUSIMAMIA MECHI YA KOMBE LA DUNIA
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Mtanzania Lina Kessy kuwa
kamishna wa mechi ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika kwa wanawake chini
ya umri wa miaka 20 kati ya Botswana na Afrika Kusini.
Mechi
hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itachezwa nchini Botswana kati ya
Oktoba 25 na 27 mwaka huu. Waamuzi kutoka Zimbabwe ndiyo watakaochezesha
mechi hiyo namba tisa.
Waamuzi
hao wataongozwa na Pamela Majo atakayepuliza filimbi wakati mwamuzi
msaidizi namba moja ni Rudo Nhananga, namba mbili ni Stellah Ruvinga na
mezani atakuwepo Tambudzi Tavengwa.
*KIONGOZI WA MWENGE AFUNGUA KITUO CHA IDYDCC
Kiongozi
wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Juma Ali Amir amefungua kituo cha kwanza
cha Football for Hope kilicho mkoani Iringa kwa kuwataka wananchi
kukituia vizuri ili wanufaike na huruma za kijamii zinazotolewa na
taasisi ya IDYDC pamoja na kuendeleza mpira wa miguu.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi wa kituo hicho jana (Oktoba 13 mwaka huu), kiongozi
huyo amesema taasisi ya IDYDC (Iringa Development of Youth, Disabled and
Child Care) wamefanya vizuri kuamua kutumia mpira wa miguu kusaidia
jamii kwa kuelimisha juu ya mambo mbalimbali kama ugonjwa wa ukimwi,
kusaidia walemavu, haki za watoto na afya ya jamii.
Naye
Mwakilishi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Patrick
Onyango amesema amefurahishwa na kukamilika kwa kituo ambacho
kitasaidia jamii.
Amesema
idadi kubwa ya watu waliofika kwenye uzinduzi huo inadhihirisha ni
kiasi gani kituo hicho kitakuwa na matokeo mazuri kwa jamii.
Onyango
alisema hicho ni kituo cha 14 kukamilika kati ya 20 vinavyojengwa
barani Afrika ikiwa ni mpango wa FIFA kurudisha kwa jamii mafanikio
iliyopata kwenye fainali za kwanza za Kombe la Dunia barani Afrika.
Kituo
hicho kina uwanja mdogo wa mita 20 kwa 40 uliowekwa nyasi bandia, jengo
lenye ukumbi wa mikutano kwa ajili ya semina, chumba cha kupimia
ukimwi, chumba cha ushauri nasaha, maktaba na ofisi.
Zaidi ya dola 270,000 za Marekani zimetumika kukamilisha ujenzi wa kituo hicho kilicho eneo la Mtwivila, Iringa mjini.
Post a Comment